NA MADINA ISSA

WIZARA ya Afya imesema itaendeleza mikakati ya upatikanaji wa huduma za afya katika vituo vya afya na hospitali zote Unguja na Pemba, ili kuwapunguzia usumbufu wananchi wakiwemo wazee.

Naibu Waziri wa Afya, Harusi Said Suleiman, aliyasema hayo wakati akizungumza na wazee katika maadhimisho ya siku ya afya duniani, yaliyofanyika ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi Kikwajuni.

Lengo la maadhimisho hayo ni kutathmini namna wazee wanavyoweza kusaidiwa katika masuala ya afya na huduma nyengine stahiki kwa mujibu wa mazingira yao.

Alisema wazee wenye umri unaoanzia miaka 60 wanakabiliwa na maradhi zaidi ya matatu na wanapata usumbufu wanapofuata huduma za afya.

Hivyo, alisema changamoto hiyo itaondolewa kwa kuhakikisha huduma katika vituo vya afya na hospitali zinaimarishwa mara dufu.

Aliwashauri wazee kuwa utaratibu wa kufanya mazoezi ili kukabiliana na maradhi yanayowasumbua.

Aidha aliziomba familia kuwapa huduma muhimu wanazostahiki wazee, kuwa karibu nao na kuwaonesha upendo.

“Tukumbuke wazee wetu tuna wajibu wa kuwaenzi kama walivyotutunza sisi wakati tukiwa wadogo,  tukiwadharau na sisi tutadharauliwa na watoto wetu wakati tutakapokuwa wazee,” alisema.

Aliwakumbusha wazee kuwa na utaratibu wa kufika katika vituo vya afya vilivyoko karibu yao ili kupata matibabu na ushauri juu ya afya zao.

 

Alitoa wito kwa taasisi zinazoshughulikia wazee kuongeza juhudi na kutoa huduma kwa upendo ili wazee waridhike na huduma wanazopata.

Mapema Katibu wa jumuiya ya wastaafu na wazee (JUWAZA) Salama Kombo, alisema kwa mujibu itifaki ya Umoja wa Afrika, Afrika ina wazee milioni 64 na watafikia milioni 212 ifikapo mwaka 2050.

Hivyo aliiomba serikali kutayarisha mazingira ya uzeeni mapema ili itakapofikia wakati huo kusiwe na mzigo mkubwa wa kuwatunza wazee.

Akitoa salamu za wazee, mzee Juma Wakili, alimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein kwa kuendelea kuwaenzi wazee.

MAONI YAKO