NA MWANDISHI WETU

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan, ameondoka nchini jana kwenda London, Uingereza kushiriki mkutano wa wakuu wa Serikali wa Jumuiya ya Madola (CHOGM) unaotarajiwa kuanza leo hadi Aprili 20 mwaka huu, akimwakilisha Rais, John Pombe Joseph Magufuli.

Mkutano huo ambao kaulimbiu yake ni “Kuelekea Mustakabali wa Pamoja” utafanyika chini ya uenyekiti wa Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May na utafunguliwa na Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Malkia Elizabeth wa Pili wa Uingereza.

Majadiliano ya mkutano wa CHOGM 2018 yatajikita kwenye maeneo manne makuu ya kipaumbele ambayo yatajadili namna Jumuiya ya Madola inavyoweza kufikia mustakabali wenye ustawi zaidi; mustakabali endelevu zaidi; mustakabali wenye haki zaidi; na mustakabali wenye usawa zaidi.

Mijadala katika maeneo hayo itahusisha masuala mbalimbali ikiwemo, kukuza zaidi biashara na uwekezaji baina ya nchi za Jumuiya ya Madola kwa manufaa ya nchi wanachama na jumuiya nzima; kukuza na kuendeleza misingi ya demokrasia; ajenda ya mabadiliko ya tabianchi na maendeleo endelevu pamoja na masuala ya uhalifu wa kimataifa kama vile ugaidi, uhalifu wa kimtandao na usafirishaji wa binadamu.

Jumuiya ya Madola ilianzishwa mwaka 1949 kupitia tamko la London ambalo lilikuwa ni matokeo ya mkutano wa Mawaziri Wakuu wa nchi za jumuiya hiyo.

MAONI YAKO