HAKUNA kitisho kikubwa cha kupoteza maisha kwa wanawake visiwani Zanzibar kwa wakati huu, kama kukumbwa na maradhi ya saratani ya shingo ya mlango wa kizazi.

Tatizo la ugonjwa huo haliko Zanzibar pekee kwani takwimu za kidunia zinaonyesha kuwa zaidi wanawake 260,000 kwa mwaka kutoka na ugonjwa huo.

Zanzibar nayo haiko salama dhidi ya ugonjwa huo kwani tatizo la saratani ya shingo ya mlango wa kizazi, limekuwa likiongezeka mwaka hadi mwaka.

Kwa mujibu wa takwimu kutoka wizara ya Afya, kati ya wanawake 392 waliofanyiwa uchunguzi wa maradhi hayo katika hospitali Mnazimmoja mwaka 2016, watu 90 walibainika kuwa ugonjwa huo.

Hali ilikuwa mbaya zaidi katika mwaka 2017, kwani kati ya wanawake 560 waliofanyiwa uchunguzi, 140 waligunduliwa na saratani hiyo, ambayo ni ugonjwa usioambukiza.

Kutokana na hali hiyo, ambayo inasababisha kuwapoteza mama, dada, shangazi na wapendwa wetu, serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuja na mkakati wa chanjo dhidi ya saratani hiyo kwa wasichana wenye umri wa kati ya miaka 9 hadi 14.

Kwa hakika hatua ya serikali ya Mapinduzi kuleta chanjo ya saratani ya shingo ya mlango wa kizazi ni kukihakikishia kizazi kijacho kuwa salama dhidi ya maradhi hayo.

Tungependa kuieleza jamii kwamba saratani ni maradhi hatari yenye kutesa na kuumiza mwili, lakini baya zaidi ni kwamba matibabu yake yana gharama kubwa na yasio na uhakika sana hasa pale inapogunduliwa ikiwa kwenye hatua za mwisho.

Mara ngapi tumeziona familia zenye wagonjwa wa saratani ambapo hulazimika kuingia kwenye umasikini kutokana na kugharamika dhidi ya  matibabu ya saratani.

Kwa sababu jamii yetu haina utamaduni wa kupima afya, hapa Zanzibar wanawake wengi hubainika kuwa na saratani hiyo ikiwa kwenye hatua za mwisho za kuchukua uhai wa mgonjwa.

Ni vyema sana pale inapotokezea neema kama hii inayoletwa na serikali, jamii ikahakikisha unaunga mkono kwa sababu baada ya yote kinacholengwa ni kujikinga na maradhi hayo.

Tungependa kuihakikishia jamii kuwa kwa mujibu wa wataalamu chanjo hiyo wanayopewa wasichana ni salama na isiyo na shaka yoyote na kinga muhimu kwa mustakbali wa maisha yao ya baadae dhidi ya saratani hiyo.

Hata hivyo, pamoja na chanjo hiyo, jamii inapaswa kuhakikisha kuwa inafuata maelekezo ya wataalamu wa afya yale yanayotuongoza jinsi ya kuepukana na  magonjwa ya saratani.

Kwa mfano, umefika wakati jamii kike kwa kiume kuepuka uvtaji wa sigara pamoja na bidhaa za tumbaku ambazo zinaelezwa kuwa ni kichocheo kikubwa cha saratani.

Ni vyema jamii ikahakikisha ina kula chakula chenye afya, wanawake wneye watoto kuwanyonyesha hali ambayo inaelezwa kuwa inapunguza hatari kwa mama kuugua saratani hiyo.

Aidha kama tunavyosisitizwa na wataalamu wa afya ni muhimu kufanya mazoezi, kuacha pombe na kufanya uchunguzi wa mara kwa mara.

MAONI YAKO