UTALII umefikia hatua ya kuwa sekta kiongozi kwa uchumi wa Zanzibar, ambapo umekuwa tegemeo kubwa visiwani hapa baada ya kuanguka bei kwenye soko la dunia kwa zao karafuu.

Utalii visiwani Zanzibar umefukia hatua ya ule msemo wa maarufu ni kama uji na mgonjwa, kwa maana kwamba bila ya utalii uchumi wa Zanzibar, utaingia kwenye mgogoro mkubwa.

Kwa mujibu wa taarifa za karibuni kabisa, sekta hiyo inaiingizia Zanzibar zaidi ya asilimia 70 ya fedha za kigeni, huku ikiwa na mchano mkubwa kwenye pato la taifa sambamba na kuongoza utatuzi wa janga la ajira.

Hata hivyo jamii yetu inapaswa kuelewa kuwa watalii wanapotoka katika nchi zao na kutembelea katika mataifa yetu huwa wanakuja kuangalia vitu adimu ambavyo wao hawana ila katika nchi yetu tumejaaliwa kuwa navyo.

Kwa mfano, watalii wanaokuja Zanzibar, wanapendezwa na vitu vingi ikiwemo hali ya hewa ambayo iko tofauti sana ikilinganishwa na katika nchi zao, pia hupenda kuja kuangalia viumbe adimu tulivyonavyo kama vile kima punju.

Aidha baadhi ya watalii huingia visiwani mwetu makusudi kuja kuangalia utamaduni wetu ikiwemo eneo kama Mjimkongwe ambalo ujenzi wa nyumba zake ni usanifu wateknolojia ya kizamani.

Utamaduni wa kizanzibari umekuwa wa kipekee kwa sababu ya mchanganyiko wa watu wake, ambao umekuwa ni adimu kuupata katika sehemu nyengine duniani.

Mchanganyiko wa watu wanaopatikana Zanzibar, ndio unaozalisha mambo ya kipekee katika jamii yetu ambayo yanatofautiana na eneo jengine duniani, kwa mfano suala la aina za vyakula, mavazi na hata jinsi ya watu wanavyoishi.

Hata hivyo, mambo yamekuwa kinyume sana na mategemeo badala ya utalii kuwa faida ya kifedha na kuulinda utamaduni wetu kuna mambo ambayo hayapendezi nayo yamekuwa yakijichomoza.

Utalii hivi sasa unachukuliwa kama eneo moja wapo linalochangia kuporomoka kwa maadili, ambapo hakuna tofauti ya mavazi yanayovaliwa na vijana wetu na watalii wanaotoka maeneo mbalimbali ulimwenguni.

Tunadhani wakati umefika kuwekeza zaidi kwa vijana wetu kuhakikisha wanaondokana na mila za wageni na kuzitunza zile za kwetu ambazo ni sehemu ya utamaduni wetu.

Aidha kila hoteli, ni vyema vikawepo vipeperushi vyenye msisitizo kwa kila mtalii kuheshimu silka na mila za kizanzibari popote atakapokuwepo.

Kwa kufanya hivyo, tutaweza kuzuia mporomoko wa maadili unaochangiwa na watalii kutofahamu umuhimu wa mila zetu.

Tunadhani pia kufanya hivi kutasisitiza haja ya kuwa na Zanzibar yenye historia ya dini na maeneo ya kuvutia sambamba na tamaduni nyengine kadhaa.

Tusiifanye Zanzibar kuwa ni sehemu ya vitega uchumi kuwa ndio vivutio vikubwa tukasahau utamaduni wa kidini ambao ndio uliobeba ustaarabu wa Wazanzibari.

MAONI YAKO