BAADA ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar awamu ya saba kuingia madarakani, Rais Dk. Ali Mohamed Shein alianzisha utaratibu wa mawaziri kuzungumza na waandishi wa habari kila baada ya miezi mitatu.

Dk. Shein yeye mwenyewe Rais akiwa kiongozi mkuu wa nchi, alikuwa mfano wa kutekeleza utaratibu huo, uliolenga kutoa ufafanuzi juu ya utendaji wa wizara, mikakati ya maendeleo, mafanikio na changamoto mbalimbali.

Mpango huo haukuishia kwa mawaziri kutawala kumbi peke yao kwa kueleza waliyonayo, bali pia ulitoa fursa kwa waandishi kuwauliza masuala mbalimbali iwe mepesi au magumu na wao kuyatolea majibu ambayo waandishi waliyafikisha kwa wananchi kupitia vyombo wanavyovitumikia.

Waandishi waliupokea utaratibu huo kwa mikono miwili, kwani ulionesha dhahiri kwamba serikali imepania kuondoa usiri na kuendesha mambo kwa misingi ya uwazi na ukweli, jambo ambalo ni muhimu katika kutekeleza dhana ya demokrasia na utawala bora.

Katika mkutano wa kwanza wa Rais na waandishi wa habari, ofisi yake ilivialika pia vyombo vya habari kutoka Dar es Salaam, na natumai waliopata nafasi ya kuuliza masuala, walikata kiu yao baada ya kupata majibu na ufafanuzi mwanana.

Kwa sababu tuliambiwa utaratibu huo utakuwa endelevu na utafanyika kila baada ya miezi mitatu, waandishi na wananchi kwa jumla walishajenga matumaini kuwa sasa, kupitia kalamu na kamera za vyombo vya habari, watakuwa  wakipata taarifa za utendaji wa serikali yao karibu mara nne kwa mwaka kwa kila wizara.

Kwa hili hatuwalaumu viongozi wetu wakuu Rais na Makamu wa Pili wa Rais kwani wametingwa na shughili na pirika ambazo tunaamini kwa siku yenye saa 24 hawazimalizi.

Ila tunachojiuliza kwanini mawaziri wasiendeleze utamaduni huu wa kuwaita waandishi wa habari na kuzungumza nao, kwa sababu tunavyojua yapo maendeleo makubwa yaliyofanywa na serikali.

Sisi tunashinikiza kwa sababu tunaelewa umuhimu wa jamii kupashwa habari za kweli, za uhakika na zinazokwenda na wakari kuhusu maendeleo mbalimbali yaliyofikiwa na serikali yao waliyoiweka madarakani.

Tumekuwa tukijiliza sana, mbona Dk. Shein na Balozi Seif unapowaomba kwa ajili ya mahojiano hawana vigugumuzi na wala pingamizi za kuzungumza na vyombo vya habari, kwanini wasaidizi wao wawe wagumu?

Kwa mfano, huu sio kama tunawachongea hapana, lengu letu wabadilike, hivi karibuni hivi gazeti hili lilitoa toleo maalum maendeleo ya miaka saba tangu Dk. Shein aingie madarakani, tuliwatafuta baadhi ya viongozi wa wizara watupe taarifa hawakuwa tayari.

Kibaya zaidi hawakutwambia kuwa hawatotupa habari lakini kwa mwenendo ulivyokua unakwenda tulifahamu fika kuwa hawataki kutoa taarifa hizo hata hatuelewi walikuwa wakifikiri kitu gani wakati hili ndilo gazeti la kutangaza sera za serikali.

Tuseme kweli kabisa kama jambo lolote la maendeleo lililofanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar lenye manufaa kwa wananchi halikutangazwa na Zanzibar Leo, unategemea likatangazwe wapi kwengine?

Unaweza kupenda redio na televisheni, lakini wakeshatangaza na kuonyesha hewani maana yake taarifa hizo nazo zimepeperuka bila ya hata kuwepo rekodi ya kudumu ya muda mrefu.

Umefika wakatu viongozi wawe mstari wa mbele kupenda, kuvitunza na kuvithamini vya kwao kama kuna changamoto milango iko wazi ya kujadiliana na kushauriana kwa kuelewa kuwa hakuna mkamilifu.

Lengo letu tuione Zanzibar inakwenda mbele huku wananchi nao wakielezwa kwa uwazi mambo yote yenye mustakabili wa maisha yao kwa sababu wao ndio walioiweka madarakani serikali yao.

Tunashauri utaratibu wa viongozi wa wozara wa kuzungumza na waandishi wa habari urejeshwe.

MAONI YAKO