NA MWANDISHI WETU

PENGO la pointi tatu zilizokuwa zimesalia ili kuifikia Simba kileleni iliyo nafasi ya kwanza kwenye ligi msimu huu hatimaye limezibika kufutia ushindi wa Yanga dhidi ya Stand United jioni ya jana.

Ikicheza kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga imeibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Stand United na kuwafanya wafikishe pointi 46 sawa na vinara Simba, ingawa wanasalia kileleni kutokana na faida ya mabao mengi ya kufunga.

Alikuwa ni Yusuph Mhilu aliyefanya kazi nzuri mapema dakika ya 6 ya mchezo, kazi iliyosababisha beki wa Stand, Ally Ally, kujifunga kufuatia kupiga krosi nzuri kulia mwa uwanja na kuzaa bao.

Dakika ya 11, kiungo aliyewahi kuichezea Simba, Ibrahim Ajib, alifunga bao la pili na kufanya ubao wa matokeo usomeke 2-0.

Mpaka dakika 45 za kwanza zinamalizika, Yanga walikuwa mbele kwa mabao hayo mawili.

Kipindi cha pili kilipoanza, Stand walimiliki mpira kwa asilimia kubwa wakipambana kutafuta mabao, ambapo juhudi zao zilizaa matunda kwa Vitalis Mayanga kufunga katika dakika ya 83.

Ilichukua dakika mbili pekee Obrey Chirwa akaiandikia Yanga bao la 3 kwenye dakika ya 85 na kufanya mchezo uende mpaka dakika 90 na kumalizika, matokeo yakiwa ni mabao 3-1.

Matokeo hayo yameifanya Yanga ilingane kwa alama na vinara wa ligi, Simba kwa kuwa na alama sawa ambazo ni 46, japo Simba wana mchezo mmoja mkononi.

MAONI YAKO