NA MWANDISHI WETU

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA), imesema Benki ya Dunia (WB), haihusiki na ujenzi wa bandari na matangi yatakayotumika kushushia na kuhifadhia mafuta huko Mangapwani.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mamlaka hiyo, benki hiyo ilidhamini kazi ya upembuzi yakinifu wa awali wa ujenzi wa bohari, bandari ya mafuta na gesi katika eneo hilo.

Taarifa hiyo pia ilieleza kuwa benki hiyo itadhamini upembuzi yakinifu wa ujenzi wa bohari na bandari hiyo ya mafuta na gesi katika eneo hilo.

Hivi karibuni akizungumza na gazeti hili, ofisa Uhusiano wa ZURA, Hassan Juma Amour, alisema tayari wameshashirikiana na wadau mbalimbali wanaohusika na bandari pamoja na wakusanyaji kodi, kwa ajili ya matayarisho ya ujenzi huo.

Alifahamisha, iwapo bandari hiyo itakamilika itawarahisishia wananchi kupata huduma hiyo muhimu katika ustawi wa maendeleo ya maisha yao, kutokana na kuagizwa kutoka nje moja kwa moja.

Alisema, eneo litakalotumika hivi sasa ni kubwa na lenye kujitosheleza kutokana na kima kikubwa cha maji na litakuwa ni eneo zuri kwa uchumi wa Zanzibar.

MAONI YAKO