MSHAMBULIAJI wa timu ya Black Sailor Hassan Said (kulia) akiwania mpira na kipa wa Kilimani City Yussuf Ali, wakati timu hizo zilipokutana kwenye mchezo wa Ligi Kuu Zanzibar uwanja wa Amaan jana, mchezo ambao ulimalizika kwa sare ya kutofungana .

NA NASRA MANZI

MAAFANDI wa Polisi wameendelea kugawa pointi baada ya jana kukubali kipigo cha mabao 3-0, kutoka kwa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Zanzibar timu ya JKU.

Mchezo huo wa Ligi Kuu Zanzibar ulipigwa jana katika uwanja wa Amaan majira ya saa 8:00, ambao ulikuwa mzuri na kupendeza kwa muda wote.

JKU ilianza mchezo kwa kupanga ,mashambulizi langoni mwa Polisi  ili kutafuta bao la mapema, juhudi ambazo zilifanikiwa kuandika bao la kwanza dakika ya 16 lililofungwa na Suwedi Juma.

Baada ya bao hilo Polisi walikuja juu  kutafuta bao la kusawazisha lakini walijikuta wakipachikwa bao la pili lililofungwa tena na mchezaji Suwed Juma dakika ya 36, ambayo yalidumu hadi kipindi cha kwanza kinamalizika.

Kipindi cha pili kila timu ilirudi na kasi mpya  kwa lengo la kupata mabao, Polisi wakitaka kusawazisha na JKU ikitaka kuongeza jingine  lakini washambuliaji wa pande zote walikosa mabao ya wazi.

Hata hivyo JKU waliongeza bao la tatu la dakika ya 80 baada ya mchezaji wa Polisi Juma Ramadhani kujifunga katika harakati za kutaka kuokoa.

Huo ni mchezo wa pili kwa Polisi kupteza ambapo wiki iliyopita ilikubali kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa KVZ.

Mbali na mchezo huo, mchezo mwengine ulipigwa majira ya saa 10:30 jioni baina ya Mabaharia weusi na Kilimani City, mchezo ambao ulimalizika kwa wanaume hao kugawana pointi  kwa kutokufungana.

 

MAONI YAKO