NAIBU Spika wa Baraza la Wawakilishi, Mgeni Hassan Juma, akizungumza wakati wa kuahirishwa kwa bunge la vijana Zanzibar lililofanyika katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani ambao bunge hilo lilijadili mambo kadhaa yanayowahusu vijana ikiwa ni kuadhimisha siku ya Jumuiya ya Madola Duniani.(PICHA NA OTHMAN MAULID).

Mgeni asema limedhihirisha ubora

NA KHAMISUU ABDALLAH

NAIBU Spika wa Baraza la Wawakilishi, Mgeni Hassan Juma, amesema uwepo wa bunge la vijana umeonesha umahiri mkubwa katika kujenga hoja mbalimbali na uwezo wao kuchukua nafasi za uongozi.

Alieleza hayo wakati akifunga bunge la vijana lilowashirikisha vijana 50 kutoka Unguja na Pemba katika kilele cha maadhimisho ya siku ya Jumuiya ya Madola inayoadhimishwa kila ifikapo Machi 12 ya kila mwaka duniani kote yaliyofanyika katika ukumbi wa baraza la Wawakilishi, Chukwani.

Alisema, uwezo na vipaji walivyoonesha vijana katika bunge hilo kuna haja ya kuendeleza ili kuwa na hazina ya vijana ambao watakuwa viongozi bora baadae.

“Mlichokifanya leo mmedhihirisha kwamba taifa letu lina vijana wenye vipaji na uwezo mkubwa wa kuchukua nafasi za viongozi waliopo hivi sasa katika kipindi kifupi kijacho kwani mmna vipaji vikubwa ambavyo mmevionesha,”alisema.

Alisema upo umuhimu mkubwa kwa tasisi husika kuchukua juhudi za makusudi kuendeleza hazina hiyo ya taifa kwani vijana wanategemewa na ndio taifa la leo na kesho.

Hata hivyo, alisema katika kuhakikisha vipaji vya vijana vinaendelezwa ni vyema vijana nchini wakazingatiwa katika nafasi mbalimbali za uongozi hasa katika nafasi za kisiasa na ni vyema kwa vyama vya siasa kuwa na utaratibu wa kutenga nafasi mbalimbali za vijana kuingia katika vyombo vya kutoa maamuzi ikiwemo Bunge, Baraza la Wawakilishi na mabaraza ya manispaa na miji.

“Natambua kuwa baadhi ya vyama vimetenga nafasi za vijana kama CCM hivyo navisihi vyama vyengine vya siasa ambavyo bado havijawa na utaratibu huu kuiga mfano huo mzuri wa kuweka mifumo mizuri itakayowapa nafasi na fursa vijana nao katika nafasi za uongozi na kushiriki katika kutoa maamuzi yao,” alisema.

Katika hatua nyengine, alisema kutokana na vipaji na uwezo waliouonesha vijana katika bunge hilo ni dhahiri kuwa wakati wa marekebisho ya katiba ya Zanzibar utakapofika suala la nafasi za vijana inaweza kuzingatiwa katika marekebisho hayo na kutambulika kikatiba kama ilivyo nafasi za wanawake.

Alitumia fursa hiyo kuwapongeza wabunge hao wa bunge la vijana kwa kazi kubwa waliyoifanya kwa kuliendesha bunge kwa umakini mkubwa.

MAONI YAKO