NA MWANDISHI WETU

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA), imesema katika kukabiliana na tatizo la upungufu wa mafuta, imefanikiwa kuingiza lita 2.99 milioni  za mafuta ya petroli na lita 1.08 milioni za dizeli kupitia kampuni za United Petroleum (UP) na GAPGO.

Imesema mafuta hayo yameshushwa na kusambazwa katika vituo mbali mbali vya kuuzia mafuta kuanzia Februari 24 mwaka.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kaimu Mkurugenzi Huduma za Wateja wa Mamlaka hiyo, Mussa Ramadhan Haji, alisema hatua hiyo ni juhudi za serikali katika kukabiliana na tatizo la upungufu wa nishati unaolikabili taifa mara kwa mara.

Alisema tatizo la upungufu wa mafuta unaolikabili taifa, linahitaji muda kupata ufumbuzi wake kwa vile linachangiwa kwa kiasi kikubwa na ufinyu wa matangi ya kuhifadhia pamoja na uchelewaji bandarini Dar es Salaam wakati wa kupakia.

Alisema jambo la msingi ambalo wakati huu ZURA inalizingatia ni kuhakikisha mafuta mengine yanaingizwa nchini kabla ya yale yaliopo hayajamalizika.

“Hoja sio akiba iliyopo itatumika kwa muda gani, la msingi hapa ni kuhakikisha kabla hii iliyopo haijamlizika tunafanya juhudi ya kuingiza nyingine ili kuwa na matumizi endelevu,” alisema.

MAONI YAKO