WAWAKILISHI wa Zanzibar katika michuano ya Shirikisho la Soka la Afrika (CAF),JKU na Zimamoto tayari zimeshaaga michuano ya mwaka huu, baada ya kupoteza mechi zao za marudiano zilizochezwa mwanzoni mwa wiki hii.

Wakati JKU iliyotuwakilisha kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika akiiaga michuano hiyo kwa kipigo kizito cha magoli 7-0 mbele ya ZESCO ya Zambia nayo Zimamoto ilichapwa 1-0 na Walaitta Dicha ya Ethiopia.

Kuondolewa kwa wawakilishi wetu hao ilikuwa ni kama muendelezo wa kila mwaka wa kufanya vibaya kwa klabu zetu kwenye michuano ya kimataifa ambapo dalili hizo tayari zilikwishajitokeza baada ya mechi za kwanza zilizochezwa hapa nyumbani.

Kwanini tunasema hivyo,kwasababu matokeo ya sare waliyoyapata katika mechi hizo yalikuwa na dalili ya kuondolewa kutokana na kutoutumia vizuri uwanja wa nyumbani.

Ni dhahiri kwamba tumekuwa na kiu kubwa ya kupata mafanikio ya soka, kiu ya kuziona timu zetu zikicheza hatua inayofuata ya michuano hiyo yenye hadhi kubwa ngazi ya klabu.

Lakini kwa bahati mbaya tumekuwa wanyonge katika soka la kimataifa kwa kila timu tunayopangiwa kwetu sisi inaonekana ngumu hata zile ambazo mataifa yao hayana jina kubwa katika mchezo huo.

Kutokana na hali ilivyo ni wazi kwamba michuano ya mwaka huu imeshatupita na sasa tunalazimika kusubiri mwaka ujayo tukiwa na mtazamo tofauti na mipango madhubuti.
Lakini ukweli unabakia pale pale kwamba tunahitaji kwenda mbali zaidi huku tukiwa na ujasiri wa kuamini kwamba tunaweza kuvuka kutoka hatua za awali na kusogea mbele zaidi.

Kinachohitajika hapa kwanza kwa klabu zetu kujitathimni na hali tunayoendelea kuizoea ya kuwa washindikizaji wa kila mwaka bila ya kujali gharama ambazo wanaziingia katika ushiriki wao wa kimataifa.

Ni ukweli kuwa ushiriki wa kimataifa unahitaji fedha nyingi na kwa klabu za Zanzibar hili ni tatizo jengine na mara kadhaa tumekuwa tukishuhudia matafaruku katika hili.
Mara nyingi tunakuwa hatuna mipango thabiti huku soka letu likiendeshwa katika hali iliyokosa muelekeo na dira ya kutuongoza.

Lakini hapa hatukusudii kumnyooshea kidole yoyote yule,bali ni kuangalia njia za kujitathimni na kuelewa wapi tunakoelekea ikiwa hali ya sasa ya soka letu itaendelea hivi ilivyo sasa.

Kwa kipindi kirefu, ushiriki wa timu za Zanzibar kwenye michuano ya Afrika haujakuwa mzuri na kumekuwepo na dhana iliyojengeka miongoni mwa mashabiki kwamba sisi ni wa kawaida mno.

Hivyo, tunashauri umefika sasa kwa klabu na wachezaji kujitambua kwamba macho ya mashabiki na wanamichezo kwa ujumla yanawaangalia kwa kile wanachokifanya ndani na nje ya uwanja kwa maendeleo yao na nchi kwa ujumla.

Bado Zanzibar Leo tunaamini soka letu linaweza kuleta mageuzi makubwa ikiwa kila mmoja wetu atatimiza wajibu wake.

MAONI YAKO