IMEKUWA kawaida kila mwaka kuibuka taarifa za kuungua moto msitu wa hifadhi ya taifa wa Jozani, ambao ndani yake kuna viumbe adimu wakiwemo wanyama na mti.

Mara nyingi moto katika msitu huo huibuka wakati wa majira ya kiangazi ambapo kutokana na majani, nyasi na miti kuathirika na jua kali hivyo huwa rahisi sana kushambuliwa na mtoto.

Katika kiangazi cha mwaka huu kinachoendelea zipo ripoti kwamba zaidi ya hekta 19 za misitu huo wa hifadhi zimeteketea kwa moto na kusababisha hasara kubwa.

Mbali ya harasa ya kifedha iliyopatikana katika janga hilo, upo uhakika kuwa makaazi na hata baadhi ya wanyama ama baadhi ya misitu itakua imekufa  kutoka na moto huo.

Kubwa zaidi ni kwamba wanasayansi wanatueleza kuwa misitu imekuwa chanzo kikubwa cha mvua, hivyo kuathirika kutokana na moto kutaathiri mfumo wa kisayansi unaowezesha kutengenezwa kwa mvua.

Hivyo tusilalamike hata kidogo unapofika msimu wa masika ama vuli mvua zimekuwa kidogo, haziwezi kuwa nyingi kwa sababu hicho chanzo cha mvua kimeharibiwa.

Kwa mujibu wa taarifa moto huo ulioteketeza hekta hizo, umeanzia eneo la Kiungani ambalo liko katika kijiji cha Charawe ambacho ni miongoni mwa sheria zinazozunguukwa na hifadhi ya msitu.

Jambo la kusikitisha ni kwamba waliotia moto huo, tumeambiwa kuwa ni ‘watu wasijulikana’, kama hivyo ndivyo, basi itakuwa vigumu kujua sababu za kwanini wametia moto huo.

Hata hivyo, sisi tunavyoamini waliotia moto huo wanajulikana vyema na jamii ama sehemu ya jamii ya wananchi wa Charawe, ila pengine wanawalinda ili wasiweze kukabiliwa na haki kisheria inayowastahikia.

Kamwe hatuwezi kuamini na wala asitokee mtu akatuaminisha kwamba moto huo umejitia wenyewe na hilo haliwezi kutokea, hekta hizo za msitu zimeteketea kutokana na mikono ya mwanadamu.

Hili limekuwa tatizo kubwa kwenye jamii yetu na hasa huko vijijini, wananchi wanafahamu wahalifu ama wanaviona viashiria vya uhalifu, lakini wanafumba macho wakidhani hayo ndiyo mapenzi.

Tumekuwa hatupendi kuwajibishana pale makosa yanapotokea kutokana na kugandwa na ugonjwa la siku nyingi na kuyavaa makoti ya kitu kinachoitwa muhali.

Wananchi katika vijiji vinavyounda hifadhi ya msitu wa Jozani ni vyema wakafahamu kuwa kuendelea kuwaficha wahalifu wanaoutia moto msitu huo ni kulisababishia hasara kubwa taifa na kupoteza maisha ya viumbe ambavyo vyengine havipatikani sehemu nyengine yoyote duniani.

Aidha kwa tunavyofahamu msitu huo umekuwa na manufaa makubwa kwa wananchi wanaozunguuka hifadhi hiyo, kwa sababu wakulima wamekuwa wakipata fedha nyingi kila mwaka zinazotokana na shughuli za utalii katika msitu huo.

Tunachojiuliza sasa kama wengine wanautia moto kwa makusudi msitu huyo je! huo mgao wa fedha wanaopewa wakulima unaotokana na mapato ya utalii utapatikana vipi wakati wanyama na miti ambayo ni vivutio vikubwa imeshateketea kwa moto?

Vitu vyengine havihitaji elimu kubwa, lakini ni jukumu la wananchi wanaozunguuka msitu wa Jozani kufikiria mara mbili tabia ya kuwaficha wenye kuutia moto msitu huo.

Wananchi wanaozunguuka hifadhi ya msitu wa Jozani wana haki na jukumu la msingi la kuulinda msitu huo sio kwa wanaouhujumu kwa moto tu, bali hata wale wanaokata miti ovyo.

Kwa msisitizo kabisa tunapenda kueleza kuwa tuwe na tabia ya kutunza,  kuthamini na kulinda yale yanayotupatia manufaa kwa ajili ya maisha yetu ya leo, kesho na kuweka msingi mzuri kwa vizazi vijavyo.

MAONI YAKO