BAADA ya kufanikiwa kuondoshwa madarakani kwa aliekua rais wa Afrika Kusini Jacob Gedleyihlekisa Zuma kufuatia shinikizo la chama tawala cha nchi hiyo, ANC ambacho ndicho kilichopigania uhuru wa taifa hilo mwaka 1994.

Hatimae aliekua naibu wake ambae pia ni mwenyekiti wa chama hicho, Cyril Ramaphosa kunyakua nafasi ya bosi wake.

Mengi ya matarajio mema yamejengwa vichwani mwa wafuasi wa ANC wakiamini uongozi mpya wa Ramaphosa utarejesha ile historia ya mwaka 1994 ambayo ilijenga taswira njema kwa taifa la Afrika kusini.

Sambamba na kuwa na matarajio baada ya kushusha pumzi kutokana na kichapo cha muda mrefu cha utawala wa makaburu waliowanyonya wazawa wa taifa hilo wakati ule wa ubaguzi wa rangi.

Si tu kwa sumu ya ubaguzi wa rangi pekee iliyowaathiri Waafrika Kusini kwa wakati huo, bali hata kuhodhi hadhi zote muhimu na kunyimwa wazawa haki zao za msingi kwenye uongozi wa juu na nafasi nyeti za uongozi kwenye muundo wa serikali ya Afrika Kusini.

Mara baada ya uhuru wa taifa la Afrika Kusini mwaka 1994 matarajio mengi yalijengwa kwenye vichwa vya raia wa nchi hiyo walio kuwa na kiu ya kuona nchi yao inayoongozwa na Waafrika wenyewe badala ya makaburu kuondosha vilio vyao vya muda mrefu vilivyokua vimewabana wakati ule wa ulowezi.

Uongozi mpya wa Ramaphosa unatarajiwa kuakisi na kurudisha ile dhamira ya awali ya uongozi wa kwanza mweusi chini ya aliekua rais wa nchi hiyo, Nelson Mandela ambao uliimarisha uchumi wa taifa hilo.

Tukirejea kwenye historia ya wakati ule wa ukaburu nchini Afrika Kusini, tunamuona Ramaphosa alikua mwanaharakati jasiri wa maendeleo ya watu weusi ambae kwa asilimia zote aliunga mkono juhudi za aliekua mpigania uhuru wa taifa hilo, Jemedari Nelson Mandela.

Mnamo mwaka 1990 Ramaphosa aliongoza mazungumzo ya kumaliza utawala wa kibaguzi na baadaye kuwa mfanyabiashara mkubwa kabla ya kujiunga na siasa, lakini baadae aliona haja yakuongeza nguvu kwa chama chake cha ANC kwani aliamini kilihitaji busara zake.

Sasa Ramaphosa tayari amekua rais je! kwenye uongozi wake huu kama rais wa awamu ya nne wa Afrika Kusini ataweza kurejesha kwa mara nyengine imani ya wafuasi wa chama cha ANC ambayo Jacob Zuma aliipoteza?

Jacob Zuma, rais wa zamani wa Afrika Kusini

Licha ya ahadi zake kedekede alizowaahidi wafuasi wenziwe wa chama hicho cha ANC ya kwamba yupo tayari kuufufua uchumi wa nchi hiyo ambao uliporomoshwa na nguvu za ufisadi na ulaji rushwa uliofanywa na kiongozi alieondoshwa kwa nguvu madarakani, Jacob Zuma, lakini Ramaphosa anakabiliwa na changamoto lukuki za kurudisha matarajio mapya ya uchumi wa Afrika Kusini.

Wiki moja iliyopita wakati akizungumza katika moja ya vikao vya chama chake cha ANC, rais Ramaphosa aliwahakikishia raia wa taifa la Afrika Kusini kwamba atakabiliana na ufisadi wa rushwa na umasikini na kueleza kuwa ni miongoni mwa vipaumbele vyake.

Akizungumzia juu ya kuboresha sekta ya kilimo na kukuza kilimo nchini humo, Ramaphosa pia aliahidi katika moja ya vikao vyao vya kamati kuu vya ANC kwamba atarejesha ardhi muhimu ambazo zilikua mikononi mwa wasiohitajika.

Wakati huo huo alimsifu mpinzani wake wa karibu aliyembwaga kwenye kinyang’anyiro cha uenyekiti wa ANC, Nkosazana Dlamini Zuma kuwa ni jasiri na mchapa kazi.

Rais Pamaphosa alizaliwa Soweto mjini Johannesburg mwaka 1952, mnamo mwaka 1974 hadi 1976 alionja mateso ya makaburu baada ya kuswekwa kizuizini wakati akijaribu kupambana harakati za kupambana na ubaguzi wa rangi.

Mnamo mwaka 1982 aliwahi kuanzisha muungano wa kitaifa wa wafanyakazi wa migodi katika kutetea haki na maslahi ya wafanyakazi hao. Aidha mnamo mwaka 1990 ramaphosa alikua mwenyekiti wa kamati ya mapokezi ya taifa yaliyoandaa kumpokea Nelson Mandela wakati akitoka gerezani akikokua akitumikia makosa ya kisiasa kwa miaka kadhaa.

Mara baada ya uhuru wa nchi hiyo mwaka 1994, Ramaphosa alijiingiza kwenye siasa na kuwa Mbunge na Mwenyekiti wa mkutano wa kikatiba mwaka huo kabla ya kujiingiza kwenye biashara mwaka 1997 na kuwa mfanyabiashara mashuhuri nchini Afrika Kusini. Baadae mwaka 2012 alikuwa kwenye bodi ya Lonmin wakati ule wa mauaji ya wachimba migodi, tukio lililotokea kwenye mji wa Marikana nchini humo.

Baada ya sakata hilo mwaka 2014 Ramaphosa alifanyamaamuzi ya kurudi tena kwenye siasa na kukitumikia upya chama chake cha ANC baada ya kuchaguliwa kuwa makamu wa raisi wa Afrika kusini hadi mwaka jana alipochaguliwa tena kuwa Mwenyekiti wa chama hicho cha ANC.

Kwasasa rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini, anamiliki utajiri wa kiasi cha dola za kimarekani milioni 450 ambazo ni sawa na thamani ya fedha ya Ulaya (Euro) 340.

Kuchaguliwa Ramaphosa kuwa kaimu rais kwa Afrika Kusini kutampa nafasi rasmi hapo mwakani kugombea nafasi ua urasi katika uchaguzi mkuu wa nchini hiyo.

Ramaphosa kuchaguliwa kuwa rais wa Afrika Kusini, kulitokana na kuondoshwa madarakani kwa nguvu kwa aliekua rais wa nchi hiyo, Jacob Zuma baada ya kukabiliwa na shutuma za ufisadi na kula rushwa.

Jacob Zuma kwa siku kadhaa alikabiliwa na shinikizo la kutaka kuachia madaraka ya urais nchini humo kufuatia chama chake cha ANC kuwa na kauli ya pamoja ya kumuondoa madarakani hadi sakata hilo lilipofanikishwa Februari 14 mwaka huu.

Mchakato wa kuwekwa madarakani kwa rais Ramaphosa licha kuwa ulikua  na mikiki mikiki kabla ya rais aliekua madarakani, Jacob Zuma kukaidi agizo la chama chake kuodoka madarani lakini awali Chama hicho tayari kilionesha umahiri wake kwa Zuma.

Mnazimu wa ANC, Jackson Mathembu aliwahi kuzungumza kwenye bunge la Afrika Kusini na kueleza kuwa ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali nchini humo kwamba ilieleza kuwwepo tayari kumuweka raisi mwengine baada ya Zuma ambae ni Ramaphosa.

Tukio la kusinikizwa kuachia madaraka kwa rais huyo wa Zamani, Jacob Zuma (75) halikuanza jana na leo bali itakumbukwa kwamba mwezi Ogasti mwaka jana bunge la Afrika Kusini lilipiga kura ya kutokuwa na imani na rais wao Zuma.

Jaribio hilo lilitokea mara baada ya kiongozi huyo kumfuta kazi aliekua waziri wake wa Fedha, bw. Pravin Gordhan mwezi Machi mwaka jana.

Na Mwashamba Juma mwashambajuma55@hotmail.com +255776808093

MAONI YAKO