Na Ali Shaaban Juma

Donald  Trump Rais wa 45 wa Marekani  ni  mfanyabiashara maarufu nchini  Marekani  ambae ni  mmoja kati ya matajiri wakubwa duniani.  Donald Trump alizaliwa mjini New York, Marekani tarehe  14 Juni, 1946 na baada ya kumaliza masomo ya msingi na sekondari, alijiunga na Chuo Kikuuu cha Pennsylvania na kutunukiwa shahada ya uchumi.  Trump  alirithi  biashara ya kukodisha nyumba na viwanja iliyokuwa ikifanywa na bibi yake na baba yake na ndipo alipoanzisha kampuni yake iitwayo “The Trump Organization”. Trump amesimamia na kuendesha biashara hiyo tokea mwaka 1971 na mara baada ya kuapishwa kuwa Rais wa Marekani hapo Januari, 2017 aliwakabidhi  wanawe Donald Jr na Eric kuendesha biashara hiyo.

Biashara za Donald Trump zimejikita zaidi katika kujenga Hoteli, Casino, Viwanja vya mpira wa Golf na kujenga majumba marefu kwa ajili ya kukodisha makampuni ya biashara na watu binafsi. Mbali ya biashara hiyo, pia Trump amejikusanyia fedha nyingi kutokana na biashara nyengine  ambapo hadi kufikia mwaka 2017, Trump alikuwa ni mtu wa 544 kwa utajiri duniani akiwa na jumla ya Dola Bilioni 3.5.

Kwa mujibu wa maelezo yake binafsi, Donald Trump alianza biashara kwa mtaji wa Dola Milioni moja alizikopa kutoka kwa baba yake ambapo hadi kufika mwaka 1982 tayari alikuwa na mtaji wa Dola Milioni 200. Alipotangaza nia ya kuwania Urais wa Marekani hapo tarehe 16 Juni, 2015, Trump alitoa ukurasa mmoja wa taarifa ya benki uloonesha kuwa alikuwa na mali zenye thamani ya Dola Bilioni 8.7. Mradi mkubwa wa kwanza wa Donald Trump ulikuwa ni mwaka 1978 aliponunua Commodore Hotel katika mji wa Manhattan na kutumia jumla ya Dola Milioni 70 kuifanyia matengenezo hoteli hiyo.

Katika mwaka huo huo wa 1978, Donald Trump alikamilisha mazungumzo ya kujenga jengo liitwalo “Trump Tower” lenye ukubwa wa ghorofa 58 katika mtaa wa Midtown mjini  Manhattan huko Marekani. Kutokana na ukubwa wa mradi wa jengo hilo la “Trump Tower”, majengo kadhaa madogo yalivunjwa ambapo Trump alilipa gharama zote. Mradi huo wa kujenga jengo hilo lenye ghorofa 52 na urefu wa Mita 202 ulimalizika mwaka 1983.  Jengo hili ndio makao makuu ya kampuni zote za Trump ambapo pia alitumia jengo hilo kama kituo kikuu cha kampeni alipogombea Urais wa Marekani.

Miongoni mwa watu mashuhuri waliopanga na kuishi katika jengo hilo la Bwana Trump ni pamoja na aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Soka la Marekani ya Kaskazini, Marekani ya Kusini na Visiwa vya Caribbean (North & Central America and the Caribbean Football Association) CONCACAF aitwae Chuck Blazer ambae anaishi katika fleti mbili za ghorofa ya 49 ya jengo hilo kwa malipo ya Dola 6,000/- kwa mwezi ambazo ni sawa na Shilingi 15 Milioni. Cha kufurahisha zaidi ni kwamba fleti aliyokodi mtu huyo ambayo analipia Dola 6,000 kwa mwezi anakaa paka wake tu na yeye anakaa fleti ya upande wa pili ambayo analipia jumla  ya Dola 18,000 kwa mwezi ambazo ni sawa na Shilingi 45 Milioni za Tanzania. Si hayo tu, mchezaji mashuhuri wa soka duniani, Cristiano Ronaldo  hapo mwaka 2015 alinunua fleti moja katika jengo hilo kwa jumla ya Dola 18.5 Milioni. Pia Mwana wa Mfalme wa Saudi Arabia aitwae Mutaib bin Abdulaziz bin Saud pia amekodi fleti ya kuishi katika jengo hilo.

Pia Donald Trump alidhamini matengenezo ya bustani ya mapumziko iitwayo Central Park katika mtaa wa Wollman Rink ambapo jumla ya Dola Milioni 1.95 zilitumika kutengeneza bustani hiyo kwa makubaliano kuwa Trump awe na haki ya kutumia sehemu ya bustani hiyo kwa shughuli zake binafsi.

Katika mwaka 1988, Trump alinunua Plaza Hotel katika mji wa Manhattan kwa Dola 407 Milioni. Miaka sita baadae hapo mwaka 1994, Trump alilinunua na kulifanyia matengenezo jengo liitwalo “Columbus Circle” ambalo lilikuwa likiyumba na kulimiki rasmi jumba hilo baada ya matengenezo hayo.  Katika mwaka huo huo wa 1994,  huko mjini  New York, Trump alinunua jengo lenye ghorofa 44 na kuliita “Trump International Hotel and Tower”.

Miaka miwili baadae hapo mwaka 1996, Donald Trump alinunua jengo la benki ya Manhattan liitwalo “Bank of  Manhattan Trust Building”. Jengo hilo lilioko katika mtaa wa Wall mjini Manhattan lenye ghorofa 71 lilikuwa limeachwa na halitumiki. Jengo hilo, lililojengwa mwaka 1930, lilikuwa ndio jengo refu zaidi duniani kwa wakati huo.

Katika mwaka 1997, Trump alianza ujenzi wa jengo jengine pembeni ya mto Hudson alilolipa jina la “Trump Place”. Hata hivyo kutokana na hitilafu za kiufundi baadae Trump aliuza jengo hilo hapo mwaka 2005 kwa jumla ya Dola Bilioni 1.8 ikiwa  ndio jengo lililouzwa kwa bei ya juu kabisa katika historia ya jiji la New York.

Katika jiji la New York pekee, Donald Trump anamiliki  majengo makubwa kumi yote yakiwa na thamani ya Dola Bilioni 1.6.

Majengo hayo ni pamoja na lile liitwalo “40 Wall Street”  lenye thamani ya Dola  Milioni  393 liliopo katikati ya jiji la Manhattan. Jengo hilo lilikuwa likimilikiwa na aliyekuwa kiongozi wa Philippines hayati Ferdinand Marcos ambapo kwa sasa limekodishwa kwa makampuni na mashirika kadhaa. Jengo jengine kubwa la Trump katika jiji hilo la New York ni lile liitwalo “1290 Avenue of Americas” lenye thamani ya Dola 347 Milioni.  Jengo hilo  liliopo katika mtaa wa Manhattan linasimamiwa na bilionea Steve Roth ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa kampuni iitwayo Vornaldo Realty Trust.  Steve Roth alikuwa ni mmoja kati ya wapambe wakuu wa Trump katika kampeni yake ya Urais. Kitega uchumi cha tatu cha Trump katika jiji la New York ni jengo liitwalo “Trump Tower” lenye thamani ya Dola 253 Milioni.  Si hayo tu, bali pia Trump anamiliki jengo jengine la kifahari lilioko katika mtaa wa Niketown lenye thamani ya Dola Milioni 253.

Trump Ocean Club hoteli iliyoko katika jiji la Panama City nchini Panama ni moja kati ya vitega uchumi kadhaa vinavyomilikiwa na Rais wa Marekani, Bwana Donald Trump.

Jengo hilo limekodiwa na kampuni ya Nike kwa miaka 15 kuanzia  mwaka 2016 kwa malipo ya Dola Milioni 700.

Trump  Park Avenue ni jengo jengine linalomilikiwa na mwanasiasa na tajiri huyo ambalo liko katika jiji la New York  lenye thamani ya Dola 166 Milioni. Jengo hilo lina maeneo 17  ya kupangisha. Jengo hilo la “Trump Park East” lina thamani ya Dola Milioni 47  ambapo sehemu moja linakodishwa watu wa kawaida kwa ajili ya maakazi na upande wa pili yanakodishwa makampuni yanayofanya biashara. Kitega uchumi chengine kinachoingiza mamilioni ya fedha katika mfuko wa Donald Trump katika jiji la New York ni hoteli iitwayo “Trump International Hotel and Tower New York”. Jengo hilo lenye thamani ya Dola Milioni 32, mbali ya kuwa na hoteli yenye vyumba 176, lakini pia kuna sehemu  ya gereji kubwa, makaazi ya watu na ofisi zinazokodishwa.

Trump Plaza ni jengo linalomilikiwa na tajiri huyo ambalo lina thamani ya Dola Milioni 31. Sehemu ya chini ya jengo hilo linakodishwa wafanyabiashara wadogo wadogo na gereji ambapo sehemu ya juu ni fleti zinazokodishwa watu wa kawaida. Jengo jengile la rais huyo wa Marekani  ni “Trump World Tower” liliopo katika mtaa wa “845 United Nations Plaza”. Kiwanja kilichojengwa jengo hilo kilinunuliwa na Trump hapo mwaka 1997 kutoka kampuni ya United Engineering Trustee  kwa Dola 52 Milioni.  Mbali  ya kukodisha wafanyabiashara wa kawaida na gereji pia jengo hilo lenye thamani ya Dola Milioni 23 lina fleti nyingi walizokodi watu wa kawaida. Mradi  wa kumi mkubwa wa Trump mjini New York ni majengo yaitwayo “Spring Creek Towers” yenye thamani ya Dola 18 Milioni ambapo sehemu kubwa ya majengo hayo ni fleti  za kukodisha. Pia kuna hoteli yenye ghorofa 46 iitwayo Trump SOHO katika jiji hilo la New York.

Mbali ya miradi hiyo katika jiji la New York, pia tajiri huyo ambaye pia ni Rais wa Marekani ana majengo kadhaa makubwa katika miji mengine kadhaa ya Marekani na nje ya taifa hilo.

Baadhi ya vitega uchumi hivyo vya Trump katika miji mingine ya Marekani ni pamoja na Trump International Hotel iliyoko Las Vegas, Trump International Hotel and Tower iliyoko yenye urefu wa Mita 424 iliyoko Chicago na Hoteli iitwayo “Trump Towers” iliyoko katika ufukwe wa visiwa vya Sunny Isles kaskazini mwa jiji la Miami.

Jengo jengine lenye thamani ya Dola 333 Milioni linalomilikiwa na Bwana Donald Trump ni lile liliopo katika mtaa uitwao 555 California  katika mji wa San Francisco. Asilimia 33% ya jengo hilo ni fleti zilizokodishwa kwa watu wa kawaida. Hoteli nyengine yenye thamani ya Dola 52 Milioni ya kiongozi huyo wa Marekani iko katika jiji la Washington  na jengo jengine lenye thamani ya Dola 30 Milioni liitwalo “Trump Winery”  liko katika mji wa Charlottesville.

Katika mji wa Charleston huko South Dakota nchini Marekani, Trump anamiliki ghala kubwa yenye thamani ya Dola Milioni 4 ambayo inakodishwa kwa wafanyabiashara na wenye viwanda wanaohifadhi bidhaa  zao mbalimbali.

Kwa upande wa Klabu na viwanja vya mchezo wa Golf, Rais huyo wa Marekani  anamiliki viwanja kadhaa ndani na nje ya Marekani vyenye thamani ya Dola 570 Milioni. Viwanja hivyo ni pamoja na viwanja vilivyoko katika majimbo kumi ya Marekani vyenye thamani ya Dola 204 Milioni.  Kiwanja chengine na klabu ya mchezo huo wa Golf ni kile kilioko huko Malago katika mwambao uitwao Palm Beach huko Florida nchini Marekani. Ada ya kuingia na kucheza Golf katika klabu hiyo ni Dola 200,000.  Klabu hiyo ina thamani ya Dola 160 Milioni ina eneo la eka 20, saluni, vyumba vya kawaida, vyumba vya watu mashuhuri na mabwawa ya kuogelea.

Klabu  nyengine ya mchezo  wa Golf  ambayo ni mali ya Bwana Trump yenye thamani ya Dola 140 Milioni ni ile iitwayo “Trump National Doral Miami Golf Resort” iliyoko katika jiji la Miami. Viwanja viwili maarufu vya mchezo huo vilioko barani Ulaya vinavyomilikiwa na Trump ni vile vilioko nchini Scotland na Ireland vyote vikiwa na thamani ya Dola 63 Milioni.

Mbali ya vitega uchumi hivyo, lakini pia kutokana na umaarufu wa jina la mahoteli yanayomilikiwa na Bilionea huyo, Trump ameanzisha kampuni tanzu inayotoa leseni za biashara ya hoteli kwa kutumia jila lake.

Kampuni hiyo inaitwa, “Trump Hotel Management and Licensing Business”  ina thamani ya Dola 190 Milioni. Kampuni hiyo tayari imeingia ubia au kuendesha mahoteli kadhaa ndani na nje ya Marekani. Baadhi ya nchi ambazo kampuni hiyo inaendesha hoteli ni pamoja na Panama, Indonesia na Uruguay. Kampuni nyengine inayotoa leseni za biashara kwa bidhaa nyenginezo ni ile iitwayo “Trump Product Licensing” yenye mtaji wa Dola Milioni 6 inayotoa leseni ya kutumia jina la “Trump” katika bidhaa mbalimbali za kawaida.

Kwa upande wa fedha taslimu na rasilimali nyenginezo, Trump ana wastani wa fedha taslimu dola 130 Milioni ambapo alitumia jumla ya Dola 66 Milioni katika kampeni ya Urais. Jengo la mwanasiasa huyo ambalo akiishi hapo awali lenye thamani ya Dola 64 Milioni lina ukubwa wa eneo la futi za mraba 11 Elfu, ambapo pia anamiliki ndege kubwa binafsi mbili na helkopta tatu zote zikiwa na thamani ya Dola 30 Milioni. Hazina nyengine ya Bwana Trump ni nyumba binafsi ambayo wanaishi watoto wake alozaa na mke wa mwanzo aitwae Ivana. Nyumba hiyo ya kifahari yenye thamani ya Dola 30 Milioni iko katika mtaa wa Seven Springs huko Bed Ford mjini New York.

Nyumba nyengine mbili za mapumziko za Bwana Trump zenye thamani ya Dola 15 Milioni ziko katika mtaa wa matajiri  uitwao “Two Palm Beach” katika pwani ya Florida.

Vilevile Rais huyo wa Marekani kutoka chama cha Republican, anamiliki nyumba nyengine ya kuishi yenye thamani ya Dola 11 Milioni iliyoko katika Mtaa Nambari 809 North Canon Drive huko Beverly Hill. Pia katika kisiwa cha Saint Martin huko West Indies, Trump ana nyumba yenye thamani ya Dola 15 Milioni ambayo alinunua kutoka kwa mwenyeji wa kisiwa hicho ambaye alikuwa ni rafiki yake.

Majengo mengine ya Trump nje ya Marekani ni  “Trump Tower” lilioko katika mtaa wa Makati mjini Manila nchini Philippines. Jengo hilo lenye fleti kadhaa zinazokodishwa kwa watu wa kawaida ndilo refu kabisa nchini Philippines. Si hayo tu, bali pia Bilionea huyo anamiliki hoteli kubwa iitwayo. “Trump International Hotel and Tower” iliyopo mjini Toronto nchini Canada. Hoteli hiyo ya kifahari yenye urefu wa mita 277 ina jumla ya vyumba vya kawaida 260 na vyumba vya daraja ya juu 109.

Kitega uchumi chengine cha Trump nje ya Marekani ni jengo liliopo mjini Istambul nchini Uturuki lenye nafasi kadhaa zilizokodishwa kama ofisi, fleti 200 za kuishi, maduka makubwa  (Supermakerts) na sinema kadhaa.

Kitega uchumi kikubwa pekee cha Donald Trump huko Marekani ya kusini ni hoteli kubwa iitwayo  “Trump  Ocean Club” yenye vyumba vya kawaida 369, vyumba vya daraja la juu 700, eneo la kuegesha magari 1500, maduka ya rejereja, Casino, Klabu za Ufukweni, Klabu za watembea baharini kwa Viboti, Saluni za kisasa, kumbi za mazoezi ya viungo, mabwawa ya kuogelea, kumbi za mikutano na vituo vya biashara. Katika mwaka 2012, kampuni ya Sun International ilikodi eneo la futi za mraba 75,000 za hoteli hiyo kwa Dola 45.5 Milioni na kujenga mashine 600 za casino (kamari) na meza cha kuchezea kamari 32.

Hoteli hiyo ya “Trump Ocean Club”iliyomalizika mwaka 2011 ipo katika jiji la Panama City nchini Panama ina ghorofa 70 na kuchukua eneo la futi za mraba 2,500,000.  Jengo hilo liko katika eneo la Punta Pacifica na linatizama mwambao wa bahari ya Pasifiki na Guba ya Panama.

Mwandishi wa makala haya ni Mwalimu wa Chuo cha Uandishi wa Habari cha ZJMMC, Kilimani mjini Zanzibar anapatikana katika rafikifumba1@hotmail.com

MAONI YAKO