NA KHAMISUU ABDALLAH

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA), imetangaza bei mpya za mafuta huku mafuta ya petroli na ya taa yakipanda.

Akitangaza bei hizo mbele ya vyombo vya habari katika ofisi za mamlaka hizo Maisara, Ofisa uhusiano wa mamlaka hiyo, Khuzaimat Bakar Kheir, alisema bei ya reja reja ya petroli imepanda  kwa shilingi 26 kwa lita kutoka shilingi  2,230 hadi shilingi 2,256, sawa na asilimia 1.1.

Alisema bei ya dizeli imeshuka kwa shilingi 15 kwa lita kutoka shilingi 2,190 hadi shilingi 2,175 sawa na punguzo la asilimia moja.

Alisema bei ya reja reja ya mafuta ya taa imepanda kwa shilingi 25 kwa lita kutoka shilingi 1,619 kwa mwezi uliopita hadi shilingi 1,641 sawa na ongezeko la asilimi 1.35.

Kwa upande wa mafuta ya ndege, alisema mafuta hayo  yameshuka kwa shilingi 15 kwa lita kutoka shilingi 2,032 kwa lita na kufikia shilingi  2,017.

Alisema, mamlaka hiyo inapanga bei kwa kuzingatia wastani wa mwenendo wa mabadiliko ya bei za mafuta duniani.

Pia alisema ZURA imezingatia thamani ya shilingi ya Tanzania, gharama za usafiri,  bima na gharama za usafirishaji kutoka nje hadi Zanzibar.

Aidha, alisema mamlaka yao pia imezingatia kodi za serikali pamoja na kiwango cha faida kwa wauzaji wa jumla na rejareja.

Akitaja sababu zilizofanya kupanda kwa bei hizo, alisema kunatokana na kupanda kwa wastani wa bei katika soko la dunia na kupanda kwa gharama za usafirishaji.

Hivyo, aliwaambia wananchi kuwa bei zilizotangazwa na serikali ndio halali na kuwasisitiza kununua mafuta katika vituo halali ili kuepuka kuuziwa mafuta ya magendo.

MAONI YAKO