RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza kwenye hafla ya siku ya sheria Zanzibar. Maadhimisho hayo yamefanyika jana katika ukumbi wa zamani wa baraza la wawakilishi uliopo Kikwajuni mjini Zanzibar.

NA RAJAB MKASABA, IKULU

RAIS  wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema utawala wa sheria ndio dira katika utoaji haki na ndio utakaoiwezesha Zanzibar kudumisha amani na utulivu iliyopo ambayo ndio msingi wa maendeleo katika sekta zote za kiuchumi na kijamii.

Aliyasema hayo jana huko katika ukumbi wa zamani wa baraza la Wawakilishi, Kikwajuni mjini Unguja katika  hafla ya kuadhimisha siku ya sheria Zanzibar.

Alieleza kuwa utawala wa sheria ndio utakaoiwezesha Zanzibar kutekeleza mipango ya kuimarisha viwanda, kukuza sekta ya utalii, kuvutia wawekezaji, kuwa na mfumo mzuri wa biashara, kuendeleza kilimo, uvuvi na ufugaji wa kisasa pamoja na uhifadhi wa mazingira.

Aliongeza kuwa inahitajika kuwa na sheria madhubuti katika ukusanyaji wa mapato na kurahisisha ulipaji kodi, kuwa na mfumo imara wa utoaji huduma za afya, elimu pamoja na maji safi na salama.

Alisema mahakama kwa kushirikiana na vyombo vyengine vya sheria ina jukumu la kuhakikisha utendaji na uendeshaji wa shughuli zao, unapelekea kuimarika kwa hali ya amani na utulivu hasa kwa kutoa haki kwa kuzingatia misingi ya usawa na kwa mujibu wa sheria zilizopo.

“Utawala wa sheria ulio madhubuti ni ule ambao umeelekeza nguvu kubwa zaidi katika kukinga na kuzuia uvunjaji wa sheria usitokezee badala ya kujipanga katika kushughulikia kesi na mashauri yanayojitokeza na kuwasilishwa mahakamani,” alisema.

Alieleza matumaini yake kuwa mahakama itajitahidi kuchukua muda ulioelezwa katika sheria au chini ya hapo ili kuwavutia wafanyabiashara kuleta mashauri na kumaliza mashauri yao mapema.

Alisema mahakama inatakiwa kushughulikia migogoro ya ardhi, pia ni vyema kwa mahakimu wa mahkama za ardhi na mahkama kuu kutoa kipaumbele kwa migogoro ya ardhi iliyo mbele yao inayohusiana na majengo ya biashara na uwekezaji, ili isichukue muda mrefu jambo ambalo linaweza kuwakatisha tamaa wawekezaji hao.

Pamoja na hayo, alieleza kuvutiwa kwake na kauli mbiu na maudhui ya maadhimisho ya mwaka huu wa sheria inayosema “Imarisha Utawala wa Sheria kwa Kukuza Uchumi wa Nchi” sambamba na kueleza kuvutiwa na juhudi za mahakama.

MAONI YAKO