ASYA HASSAN NA MADINA ISSA

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Harouna Ali Suleiman na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud, wamesema Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  zina  katiba zake zinazojitegemea, hivyo si vyema kwa viongozi kutoa kauli zinazoweza  kuleta sintofahamu na kuivuruga jamii.

Walisema Rais wa Zanzibar ndie mwenye majukumu ya kushughulikia masuala ya Zanzibar tofauti na ilivyoelezwa na Waziri wa Sheria na Katiba, Prof. Palamagamba Kabudi, wakati akijibu maswali katika kikao kilichomaliza hivi karibuni cha bunge.

Waziri Aboud, alisema ni vyema kwa viongozi wanapozungumza masuala yanayohusu Zanzibar na muungano kuwa makini ili kutoipotosha jamii.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Said Hassan Said, alisema katiba ya Zanzibar na katiba ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania ndio misingi ya nchi hizo mbili.

Alisema tokea Zanzibar na Tanzania Bara ziungane, waasisi wa nchi mbili hizo waliheshimu muungano huo kwani kila mmoja alijua mipaka yake kikatiba.

Alisema hakuna mtu anayepinga kuwepo Rais wa Zanzibar kwani ibara ya 103 ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetambua kuwepo kwa Rais wa Zanzibar, hivyo ni jambo la kisheria na kikatiba na mipaka yake imeelezwa kwa mujibu wa kifungu cha 51 cha katiba ya Zanzibar.

Alisema kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar, madaraka yote yanayohusu masuala ya Zanzibar yatatekelezwa na Rais wa Zanzibar na anaweza kukasimu madaraka kwa viongozi wengine juu ya kutekeleza mambo yote ambayo sio ya muungano.

Mwakilishi wa jimbo la Kwamtipura, Hamza Hassan Juma, alisema mawaziri wa Zanzibar wanaongozwa na SMZ na sio SMT kama alivyodai Prof. Kabudi.

Alisema kauli nyengine kama hazitapimwa wakati zinapotolewa zinaweza kusababisha migogoro isiyo na tija.

Wawakilishi hao walisema hayo wakati wakichangia taarifa maalum iliyowasilishwa na Mwakilishi wa jimbo la Chaani, Nadir-Abdul Latif Yussuf, juu ya kauli ya Prof. Magamba aliyoitoa bungeni kuhusu madaraka ya Rais wa Muungano kwa upande wa Zanzibar.

MAONI YAKO