MWANAJUMA MMANGA NA ZAINABU ATUPAE

WAZIRI wa Biashara, Viwanda na Masoko, Balozi Amina Salum Ali, amesema biashara ya kimataifa nchini itaimarika zaidi iwapo Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS) itapatiwa nyenzo na bajeti itakayoiwezesha kuweka miundombinu imara ya uchunguzi wa bidhaa.

Alisema ZBS inapaswa kuwa na majengo ya kisasa yenye hadhi ya taasisi hiyo na vifaa vya maabara vinavyolingana na ukuaji wa teknolojia.

Aliyasema hayo katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mwenyekiti wa bodi ya ZBS,  Prof. Ali Seif Msimba, katika semina  juu ya umuhimu wa viwango na bidhaa zenye ubora katika maendeleo ya jamii na kiuchumi kwa wajumbe wa Kamati ya Fedha, Biashara na Kilimo ya Baraza la Wawakilishi.

Hivyo aliwaomba wajumbe kuunga mkono maendeleo ya ZBS kwa kuhakikisha inawezeshwa kibajeti na kupatiwa ushauri wa kitaalamu utakaosaidia kufanya kazi zake kwa ufanisi.

Aidha aliwaomba kutoa miongozo juu ya ZBS inavyohitaji kuimarishwa ili bidhaa zinazoingia nchini   ziwe na viwango stahiki na kulinda afya ya mtumiaji.

Alisema ZBS ni umuhimu katika maisha ya kila siku ya mwananchi hivyo inahitaji kuimarishwa na kuwa na uwezo wa kufanya uchunguzi wa kimaabara kwa bidhaa zote zinazoingizwa nchini.

Alisema ZBS imeanzisha kamati 19 za kiufundi ambazo zina wataalamu kutoka taasisi za umma na binafsi, vyuo vikuu, wenye viwanda na wazalishaji wengine ili kuhakikisha kazi inayofanywa inakuwa na ubora.

Alisema kamati hizo zimepewa majukumu ya kuandaa viwango vinavyotumika katika kuthibitisha ubora wa bidhaa, ambapo jumla ya viwango 143 vya Zanzibar vimeidhinishwa.

Aidha alisema hadi sasa kampuni 24 zimewasilisha maombi ya kutumia alama ya ubora ya ZBS ambapo bidhaa 31 zimeombewa matumizi ya alama hiyo.

Nao wajumbe wa kamati hiyo, waliiomba taasisi hiyo kuwalinda wakulima juu ya matumizi ya dawa zisizo na ubora ambazo zinasababisha kutopata mazao mengi.

Akifunga semina hiyo, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Yussuf Hassan Iddi, aliitaka ZBS kutovunjika moyo katika kufanya kazi zake na kwamba kamati hiyo itaipa ushirikiano kila inaouhitaji.

MAONI YAKO