NA KHAMIS AMANI

WAFANYAKAZI wa hoteli ya Zanzibar Beach Resort iliyopo Mazizini, wataanza kufaidika na mishahara mipya iliyotangazwa na serikali, kuanzia Disemba mwaka huu.

Meneja wa hoteli hiyo, Rajesh Kumar Roy, alisema hayo wakati akizungumza na gazeti hili ofisini kwake, kufuatia malalamiko ya  wafanyakazi kudai ukiukwaji wa agizo la serikali la kulipwa mishahara mipya kwa taasisi binafsi.

Alisema kuchelewa kuwalipa wafanyakazi wake mishahara mipya iliyotangazwa na serikali, kulitokana na tathmini waliyokuwa wakiifanya juu ya mapato ya hotelini.

Alisema hivi sasa uongozi wa hoteli hiyo pamoja na wanasheria wamekaa kufanya tathmini hiyo na kukubaliana, hivyo kuanzia Disemba mishahara hiyo italipwa.

Kabla baadhi ya wafanyakazi wa hoteli hiyo waliulalamikia uongozi wao kwa kutowalipa mishahara mipya iliyotangazwa na serikali.

Walidai ni zaidi ya miezi mitatu imepita tokea serikali ilipotoa agizo hilo, lakini viongozi wa hoteli hiyo hawajawalipa hadi sasa.

Walidai wanashangazwa kuona hoteli kubwa kama hiyo kutowalipa mishahara hiyo wakati kuna hoteli ndogo zimeanza kutekeleza agizo hilo.

Walisema hali hiyo inaonyesha dhahiri uongozi huo kutotii agizo la serikali kwa makusudi, hali inayoweza kusababisha utendaji mbovu hotelini hapo.

Hata hivyo, Kumar alisema uongozi haujawatelekeza wafanyakazi bali inawajali kwani wao ndio watendaji wakuu wa kuiingizia mapato.

Aidha alisema uongozi pia utahakikisha unawapatia haki na fursa wafanyakazi wake ili kuleta mapenzi ya kiutendaji pamoja na kukabiliana na ugumu wa maisha.

MAONI YAKO