NA HAFSA GOLO

MKUU wa miradi katika taasisi wa Milele Foundation, Khadija Ahmeid Sharif, amesema wamejipanga kubadilisha namna ya ufundishaji kwa walimu wa Zanzibar hususan katika masomo ya sayansi.

Alieleza hayo katika ufunguzi wa mradi maalum wa kushajiisha wanafunzi wanawake kusoma masomo ya sayansi na kutayarishwa kwenye mazingira ya kutumia fursa za ajira nchini.

Alisema mpango huo utasaidia upatikanaji wa wataalamu wengi, ambao watasaidia kuimarisha maenndeleo ya taifa na kupunguza changamoto ya uchache wa wataalamu.

Aidha alisema mpango huo pia utawasaidia walimu  kuongeza  mbinu rafiki za ufundishaji ambazo zitasaidia kuwajenga wanafunzi kupenda masomo ya sayansi.

Aidha alisema mradi huo kwa awamu ya kwanza utashirikisha  skuli 15 za serikali Unguja na Pemba na walimu 75 huku wakiwafikia wanafunzi zaidi 300.

Kuhusu lengo la mradi huo, alisema umelenga kuleta mabadiliko ya ufundishaji wenye kuangalia zaidi masomo ya vitendo kuliko nadharia ili wanafunzi wawe na uelewa zaidi katika masomo hayo kwa kutumia vifaa vitakavyosaidia kuwapatia ujuzi wenye tija zaidi.

Nae Mkuu wa skuli ya elimu ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) Dk. Maryama Jaffar Ismail, alisema katika mradi huo kutakuwa na mitaala maalum itakayowawezesha walimu kufundisha kwa mahitaji ya sasa  na ya baadae ambapo dunia inaangalia ulimwengu wa sayansi na teknolojia.

Alisema hatua hiyo itasaidia  walimu  kufundisha katika mazingira stahiki ili wanafunzi wanawake wawe na uwezo utakaowawezesha kuwa wabunifu, na kuondosha dhana kwamba masomo ya sayansi zaidi husomwa na wanafunzi wanaume.

MAONI YAKO