NA MWANDISHI WETU, MACHAKOS

KIKOSI cha Zanzibar Heroes, leo kitatupa karata yake ya pili kwenye michuano ya Kombe la Chalenji dhidi ya ndugu zao wa Kilimanjaro Stars, katika uwanja wa Kenyatta mjini Machakos.

Heroes juzi iliitandika Rwanda magoli 3-1 katika mchezo wa kwanza na hivyo kujijengea matumaini bora ya kusonga mbele hatua inayofuata.

Kikosi hicho leo kitashuka uwanjani kikihitaji ushindi mwengine ambao utawaweka kwenye nafasi ya kutinga nusu fainali,lakini, wakikabiliwa na upinzani kutoka kwa Kili Stars ambayo ililazimishwa sare ya 0-0 na Libya kwenye mchezo wa ufunguzi.

Hata hivyo,Kocha wa Heroes, Hemed Suleiman ‘Moroco’, amesema, wana kila sababu ya kushinda mchezo huo kutokana na kiwango kizuri kilichooneshwa na wachezaji katika mechi ya Rwanda.

“Ushindi dhidi ya Kili Stars hautaki tochi, vijana wapo vizuri,tuna kila sababu ya kushinda”, alisema.

Hata hivyo, alisema, mchezo huo utakuwa mgumu kutokana na wachezaji wa timu hizo kufahamiana huku wengine wakicheza kwenye ligi moja ya Tanzania Bara.

“Ni mchezo utakaokuwa na upinzani mkubwa,lakini, mwisho wa siku sisi ndiyo tutakaotoka na ushindi”, alisema,Moroco.

Kocha Mkuu wa Kilimanjaro Stars, Ammy Conrad Ninje, amesema, tayari ameyafanyia kazi mapungufu yalioonekana kwenye mchezo dhidi ya Libya  uliofanyika juzi Jumapili.

Ninje alisema katika mchezo huo wa kwanza waliecheza katika kiwango cha kuridhisha na kikubwa alichokifanyia kazi ni kwa wachezaji wanapopoteza mpira kuweza kuutafuta kwa kila hali.

Alisema kwenye mchezo dhidi ya Libya, timu ilicheza vizuri kuanzia nyuma kupitia sehemu ya kiungo na kuunganisha sehemu ya ushambuliaji jambo ambalo limemfurahisha kwa namna timu ilivyotengeneza nafasi.

Hata hivyo,alikiri kuwa mchezo wa leo dhidi ya Zanzibar Heroes, utakuwa   mgumu kama ambavyo historia inaonesha wakati timu hizo mbili zinapokutana.

Kikosi cha Heroes kinatarajiwa ni Mohammed Abdulrahman, Ibrahim Mohammed Said, Mwinyi Hajji Mngwali, Abdallah Salum Kheri, Issa Haidari Dau, Abdulaziz Makame, Mohammed Issa Juma, Mudathir Yahya Abbas, Ibrahim Hamad Hilika, Feisal Salum Abdallah na Suleiman Kassim ‘Selembe’.

MAONI YAKO