NA ZAINAB ATUPAE

KUFUATIA kuahirishwa maandamano ya kupinga udhalilishaji yaliyokuwa yameandaliwa na Jumuiya wa Maimamu Zanzibar  (JUMAZA), Katibu Mtendaji wa jumuiya hiyo, Muhidini Zubeir, amewataka wananchi kutovunjika moyo, badala yake waendeleze mapambano dhidi ya tatizo hilo.

Hayo aliyasema wakati akizungumza na vyombo vya habari ofisini kwake Vuga.

Alisema uamuzi wa jeshi la polisi wa kusitisha maandamano yao usiwavunje moyo na badala yake waendelee kupaza sauti zao kukabiliana na maadui wanaowadhalilisha wanawake na watoto.

“Wakati tukiwa kwenye hatua za mwisho za kufanya maandamano haya tulipigiwa simu kutoka polisi kwamba wamesitisha maandamano yetu kwa kile walichodai kuhofia masuala ya usalama, lakini hatutavunjia moyo tutaendeleza mapambano dhidi ya vitendo hivi viovu,” alisema.

Hata hivyo, alisema wanaendelea kufuatilia kujua sababu za msingi zilizopeleka maandamano hayo kusitishwa hasa ikizingatiwa yalikuwa ya amani.

Alisema walipata shida kubwa ya kuwanasihi wananchi kuondoka kwenye eneo ambalo maandamano hayo yangeanzia hasa ikizingatiwa wengi walikuwa wamefikishwa kwa ajili ya kushiriki.

Naibu Katibu Mtendaji  wa Jumiya hiyo, Khamis  Yussuf, aliwashukuru viongozi na wananchi kwa kushirikiana  katika hatua zote za maandalizi ya maandamano hayo.

Akisoma risala iliyotatarajiwa kusomwa katika maandamano hayo, Halima Kassim,   alisema vitendo vya udhalilishaji vinaongezeka kutokana na viongozi kushindwa kutoa elimu kwa wananchi dhidi ya athari za vitendo hivyo.

MAONI YAKO