NA MWANAJUMA MMANGA

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman, ameitaka Kamisheni ya Wakafu na Mali ya Amana, kuchangamkia fursa ya kuanzisha mfuko wa hijja, ili kupunguza changamoto zinazowakabili mahujaji nchini.

Aliyasema hayo baada ya kukabidhiwa ripoti ya ya hijja kwa mwaka 2017, hafla iliyofanyika  Mazizini.

Alisema kama mfuko huo utaanzishwa  utasaidia wananchi kuweka fedha zao kidogo kidogo hadi zitakapolamilika kwa ajili ya kwenda kutekeleza ibada hiyo hali ambayo itapunguza changamoto za baadhi ya watu kusubiri hadi wanapostaafu kazi ndio waende kutekeleza ibada hiyo.

Alisema wanaweza kujifunza jinsi nchi nyengine zilivyofanikiwa kuanzisha mfuko huo na jinsi unavyoendeshwa.

Aidha aliitaka kamisheni hiyo kuzisimamia taasisi zinazosafirisha mahujaji ili kuondoa changamoto zinazojitokeza kila kipindi cha hija.

Alisema hatarajii kuona changamoto zilizojitokeza mwaka huu ikiwemo baadhi ya mahujaji kushindwa kwenda kutekekeza ibada hiyo, kujirea tena katika miaka ijayo.

Aliwataka watendaji wa kamisheni hiyo kujifunza kutoka nchi nyengine jinsi zinavyofanikiwa kufanikisha safari za mahujaji mwaka hadi mwaka bila vikwazo.

Alisema kuna tofauti ya ulipaji wa nauli za ndege kwa mahujaji kila mwaka hivyo alimtaka Mwenyekiti wa Umoja wa Taasisi za Hijja (UTAHIZA) kuzungumza na mashirika ya ndege ili yapunguze nauli wakati wa msimu wa hijja.

Aliwapongeza walioandaa ripoti hiyo na kwamba imewasilishwa kwa wakati na kuahidi kuifanyia kazi.

Nae Katibu Mtendaji wa kamisheni hiyo, Sheikh Abudalla Talib, ameiomba serikali kutoa ruzuku ya kutosha katika hijja ili kuimarisha huduma kwa mahujaji.

Pia aliomba kuanzishwa kamati ya kitaifa ya kiserikali ambayo itajumuisha wajumbe kutoka taasisi zenye uhusiano na shughuli za hijja kwa pande zote mbili za muungano, ili kuratibu shughuli za kisera ili kufanikisha shughuli za hijja.

Alisema kuna haja kamisheni kwa kushirikiana na na UTAHIZA na wahusika wengine  wa hijja kuandaa mongozo wa taaluma ya hijja na kupanga programu mamalum za hijja za uelimishaji kwa makundi yote ya Zanzibar na Tanzania Bara.

MAONI YAKO