Hans van der Pluijm

NA MWANDISHI WETU

KOCHA wa Singida United, Mholanzi Hans van der Pluijm, anataka kuongeza washambuliaji wawili, lakini kutoka hapa hapa nyumbani.

Pluijm, kocha wa zamani wa Yanga anaamini ana safu nzuri ya ulinzi baada ya kuruhusu mabao matano pekee katika mechi 11 za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

Lakini pia Pluijm anaamini mabao tisa ya kufunga katika mechi 11 si wastani mzuri, hivyo, anahitaji kuiongezea nguvu safu yake ya ushambuliaji hivyo amependekeza wasajiliwe washambuliaji wapya wawili.
Mkurugenzi wa Singida United, Sanga Festo, amesema, wakati Pluijm anawapa muda zaidi washambuliaji wake wa kigeni, Mnyarwanda Danny Usengimana na Mzimbabwe Michelle Katsavairo anataka kusajili wazawa wawili.

“Wachezaji wa kigeni wanapokwenda ligi mpya ni nadra kuanza na moto, hufanya vizuri msimu wa pili, hivyo, hata Pluijm bado ana imani na Usengimana na Katsavairo”, alisema, Festo.

Mkurugenzi huyo wa Singida, alisema, hata Mzambia Obrey Chirwa hakufanya vizuri msimu uliopita, lakini, msimu huu umuhimu wake umeanza kuonekana Yanga.

Singida United jana iliachana na washambuliaji wazawa, Atupele Green na Pastory Athanas huku pia ikiwatoa kwa mkopo wachezaji wake wengine wawili, Mohamed Titi na Frank Zakaria.

Singida United inashika nafasi ya nne katika msimamo wa ligi kuu wakiwa pointi 20 ilizokusanya kwenye mechi 11, ikiziwa pointi tatu na vinara, Simba.

MAONI YAKO