KIUNGO wa Zanzibar Heroes, Mohamed Issa 'Banka' (kushoto) akiwania mpira dhidi Emmanuel Imanishimwe wa Rwanda wakati wa pambano la Kombe la Chalenji lililochezwa jana.Heroes ilishinda 3-1.

Yaitandika Rwanda 3 -1

NA MWANDISHI WETU, MACHAKOS

ZANZIBAR imeanza vyema michuano ya Kombe la Chalenji baada ya kuibuka na ushindi wa magoli 3-1 dhidi ya Rwanda kwenye uwanja wa Kenyatta, Machakos nchini Kenya jana.

Kikosi cha Zanzibar Heroes kiliuanza mchezo huo vizuri na kufanikiwa kupata bao la kwanza kwenye dakika ya 35 kupitia kwa kiungo, Mudathir Yahya.

Goli hilo lilidumu hadi mapumziko na mara baada ya kuanza kwa kipindi cha pili, Rwanda walifanikiwa kusawazisha kupitia kwa Muhadjiri Hakizimana katika dakika ya 47.

Hata hivyo, Zanzibar Heroes wakazinduka tena na kufanikiwa kupata bao la pili kunako dakika ya 52 kupitia kwa Mohamed Juma.

Pamoja na kutangulia kwa magoli hayo, Rwanda ilijitahidi za kusaka bao la kusawazisha kwa kupeleka mashambulizi mfululizo langoni mwa Heroes, lakini,bahati haikuwa yao.

Heroes walipachika bao la tatu kwenye dakika ya 86, mfungaji akiwa Kassim Khamis na kuzima matumaini ya Rwanda ya kupata angalau sare kwenye mchezo huo.

Kilikuwa kipigo cha pili mfululizo ka Rwanda ambapo ilifungwa 2-0 na wenyeji Kenya kwenye mchezo wa kwanza Jumapili iliyopita.

Zanzibar itarejea uwanjani kesho kumenyana na ndugu zao Tanzania Bara, kabla ya kumenyana na Kenya hapo Disemba 9 na kukamilisha mechi zake za kundi ‘A’ kwa kucheza na Libya, Disemba 11.

Wakati huohuo,mshambuliaji wa Tanzania Bara, Mbaraka Yusuph, hataweza kucheza mechi ijayo dhidi ya Zanzibar baada ya jana kushindwa kufanya mazoezi kutokana na maumivu ya misuli.

Hayo yalithibitishwa na Kocha wa Kilimanjaro Stars, Ammy Conrad Ninje, alipozungumza na waandishi wa habari jana.

Mbaraka aliumia katika mchezo dhidi ya Libya juzi ulioishia kwa sare ya 0-0.
Ninje, alisema, katika mchezo wa kwanza walicheza katika kiwango cha kuridhisha na anataka kuangalia namna ya kuyafanyia kazi mapungufu ikiwa ni pamoja na pale timu inapopoteza mpira.

MAONI YAKO