Asema mahusiano Z’bar, Oman kuwanufaisha wananchi’

NA OTHMAN KHAMIS, OMPR

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi alisema Zanzibar na Oman zitaendelea kufanyakazi pamoja  katika dhana nzima ya kudumisha ushirikiano wa damu uliopo kwa muda mrefu kwa maslahi ya maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa jamii wa wananchi wa mataifa hayo mawili.

Balozi Seif alisema hayo alipokuwa akizungumza na na balozi mpya wa Oman nchini Tanzania, Ali Abdulla Al- Mahrouq aliyefika ofisini kwake Vuga mjini Zanzibar kujitambulisha rasmi akiambatana pia na balozi mdogo wa Oman aliyepo Zanzibar Dk. Ahmed Hamood Al – Habsi.

Alisema ushirikiano huo umeimarika zaidi kwa Zanzibar kupokea ufadhili wa vijana wake wanaopata fursa za kujiunga na masomo ya juu nchini Oman katika fani mbalimbali za mafunzo ikiwemo udaktari, uhandisi, kompyuta na lugha.

Alisema Zanzibar inafurahia kuendelea kuwepo kwa uhusiano huo wa kipekee na wa kupigiwa mfano ambao umekuwa ukileta faraja na matunda mazuri yanayotowa fursa zaidi kwa Zanzibar kutanua wigo wa kimaendeleo na kuongeza maeneo mengine ya ushirikiano wa kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni.

Balozi Seif alimueleza balozi Al-Mahrouq kwamba uungaji mkono wa Oman kwa Zanzibar hasa katika utanuzi wa Chuo cha Sayansi ya Afya Mbweni umeleta faraja kwa wananchi wengi kwenye huduma za afya zinazotarajiwa kuenea katika masafa yasiyozidi kilomita tano.

Alipongeza serikali ya Oman kwa misaada yake inayoendelea kuitoa kwa Zanzibar, hasa kwa kukubali kugharamia matengenezo ya majengo ya kihistoria ya Beit el ajab na jumba la makumbusho ya kifalme yaliyopo Forodhani.

Alisema msaada huo wa ukarabati wa majengo hayo muhimu umekuja wakati muafaka kwa vile utasaidia kuhifadhi historia ya kiutamaduni na kiutawala ya visiwa vya Zanzibar inayohusisha pia mafungamano ya majengo hayo na Oman.

Akigusia ujio wa meli ya kifalme ya Fulk Al Salamah kutoka nchini Oman, Balozi Seif alieleza kwamba Zanzibar imepata faraja kubwa ya ziara ya ujumbe wa serikali ya Oman uliowasili Zanzibar na meli hiyo ya kifahari.

Alisema wananchi wa Zanzibar wamepata kujifunza mambo mbalimbali kufuatia ujio wa meli hiyo kwa kupata taaluma ya kuepuka athari za masuala mazima yanayotokana na sekta ya mafuta ambayo kwa sasa visiwa vya Zanzibar vimo katika matayarisho ya awali ya kuendesha miradi inayotokana na sekta hiyo.

MAONI YAKO