Miswaada miwili ya sheria kuwasilishwa

NA KAUTHAR ABDALLA

MKUTANO wa saba wa Baraza la tisa la Wawakilishi Zanzibar unatarajiwa kuanza Septemba 27 hadi Oktoba 12 mwaka huu, Chukwani.

Katika mkutano huo shughuli mbali mbali zinatarajiwa kufanyika ambapo jumla ya maswali 136 yataulizwa na kujibiwa.

Hayo yalielezwa na Katibu wa Baraza la Wawakilishi, Raya Issa Mselem, alipokuwa akitoa taarifa ya shughuli za mkutano huo kwa waandishi wa habari jana.

Alisema katika kikao hicho kutakuwa na miswada miwili ya sheria ambayo iliwasilishwa na kusomwa kwa mara ya kwanza katika mkutano wa Mei-Juni, 2017 ambayo itasomwa kwa mara ya pili na kujadiliwa.

Alitaja miswada hiyo kuwa ni muswada wa sheria ya kufuta sheria ya mahakama ya kadhi namba 3 ya 1985 na kuanzisha upya mahakama ya kadhi na kuweka masharti mengine yanayohusiana na hayo.

Alisema muswada mwengine ni wa sheria ya kuanzisha Baraza la Taifa la Biashara na kuweka mambo mengine yanayohusiana na hayo.

Pia alisema shughuli nyengine ambazo zimekusudiwa kutekelezwa katika mkutano huo ni kuwasilishwa ripoti za Wizara za SMZ kuhusu utekelezaji wa maagizo ya kamati za kudumu za Baraza.

Aidha alisema shughuli nyengine ni na kupokea taarifa ya serikali kuhusu ripoti ya utekelezaji wa mamlaka ya maji Zanzibar (ZAWA) na miswaada mengine itakayosomwa kwa mara ya kwanza.

MAONI YAKO