Na Dk. Juma Mohammed, MAELEZO

WATANZANIA na hasa wale manazi wa muziki wa dansi bado wanaikumbuka ile bandi maarufu iliyowahi kutamba siku hizo Dar Jazz au almaarufu pale Jijini Dar es Salaam, kama “Majini wa Bahari” ambao waliimba wimbo wao wa “Mtoto acha kupiga mayowe, waache watu waone wenyewe”.

Wimbo huo ni kibwagizo chenye ujumbe mahsusi ambao uliotungwa na kupigwa na bendi hiyo, mwishoni mwa miaka ya sitini.

Simulizi zinaeleza kuwa Dar Jazz walitunga na kuuimba wimbo huo uliokuwa mashuhuri sana enzi zake kama kijembe kwa wapinzani wao Western Jazz (Wana Saboso) kutokana na upinzani uliokuwepo baina ya bendi hizo, kila moja ikijinadi kuwa bora kuliko mwenzake.

Agosti 11 mwaka huu, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein alipata ugeni mzito, ugeni huo ni Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola Patricia Scotland.

Ujio wake umedhihirisha uhusiano wa Zanzibar ni mzuri na Jumuiya ya Madola na ni kielelezo tosha cha kukubalika na kuungwa mkono kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ya awamu ya saba inayoongozwa na Rais Dk. Ali Mohamed Shein kimataifa.

Katika mahojiano mafupi na waandishi wa habari mara baada ya kumaliza mazungumzo rasmi na Rais wa Zanzibar Dk. Shein, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, amesema wamevutika kuja Zanzibar kutokana na kushamiri kwa demokrasia, utawala bora, uwajibikaji na juhudi za kukuza uchumi.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola amesema kwamba hali ya amani na utulivu aliyoiona Zanzibar inatia faraja Jumuiya yao na yeye binafsi amevutika sana na visiwa vya Zanzibar kwa utulivu wake.

“Nina bahati kubwa kufika Zanzibar, ni visiwa tulivu sana na kwa kweli naipongeza serikali, na nakupongeza wewe Mhe. Rais Dk. Shein sisi tupo pamoja nanyi katika jitihada zenu kuwatumikia wananchi”, alisema Katibu Mkuu huyo.

Amesema amekuja Zanzibar kuja kushirikiana na Serikali na kwa sababu hiyo katika mazungumzo yao wamezungumzia namna Jumuiya ya Madola itakavyoweza kusaidia katika sekta ya elimu na masuala mengine.

“Kwa hakika nimefurahi sana, nimepokelewa vizuri nataka kusema kwamba nimekuja hapa kushirikiana na Serikali na sisi (Jumuiya ya Madola) Zanzibar inafanya vizuri sana kupambana na vitendo vya udhalilishaji, tunawaunga mkono”,amesema Patricia Scotland.

Amesema kuna miradi kadhaa ambayo Zanzibar inaweza kunufaika nayo na kwa kuwa sauti ya Zanzibar, Sauti ya Tanzania ni yenye kusikika na kuheshimika katika Jumuiya anaamini kila kitu kitakwenda vizuri na wananchi wanafurahia juhudi za Serikali yao.

Jumuiya ya Madola imeridhika na utendaji kazi wa Rais Dk. Shein katika kuwatumikia wananchi wa Zanzibar na kwa sababu hiyo, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola Patricia Scotland wataiunga mkono Zanzibar katika sekta ya elimu, afya na utawala bora.

KATIBU Mkuu wa Umoja wa Madola, Patricia Scotland akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumaliza mazungumzo yake na Dk. Shein Ikulu mjini Zanzibar.

Awali, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dk. Ali Mohamed Shein alisema kwamba katika mazungumzo yao, wamezungumzia masuala mbalimbali ya kijamii, kiuchumi ambapo Jumuiya ya Madola imeipongeza Zanzibar kupambana na udhalilishaji, lakini pia namna inavyotoa fursa kwa vijana na akinamama katika nyanja mbalimbali.

Rais Dk. Shein amesema kwamba huu ni ugeni mzito na ni jambo kubwa kwa Zanzibar kwani yeye amekuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa miaka tisa, lakini hajawahi kupata ugeni wa aina hiyo, hivyo ni ugeni muhimu kwa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Jumuia ya Madola ni ushirikiano wa hiari wa nchi zilizo na mamlaka sawa ya kiutawala zilizoungana kushughulikia mambo kadhaa ya muhimu ikiwa ni pamoja na mapambano dhidi ya rushwa.

Malkia Elizabethi II ndiye Mkuu wa Jumuia ya Madola. Sekeritariati ya Jumuia ya Madola ndiyo hushughulika na uendeshaji wa shughuli za Jumuia siku hadi siku na inaongozwa na Katibu Mkuu ambaye huchaguliwa na wanachama wa Jumuia ya Madola. Makao makuu ya Jumuia ya Madola yako Marlborough, Uingereza.

Jumuiya ya Madola ilianzishwa karne ya 19 kushirikisha makoloni ya Uingereza. Mwaka 1949 chini ya himaya ya kifalme, nchi huru zilihusishwa. Toka 1973 mikutano ya wanajumuiya imefanywa kila baada ya miaka miwili chini ya Malkia Elisabeth II

Masharti ya kujiunga na Jumuia ya Madola ni pamoja na kwamba nchi iwe imewahi kutawaliwa na Uingereza moja kwa moja au kwa namna nyingine, au nchi iwe na uhusiano  wa kiutawala na nchi ya Jumuia ya Madola, au nchi iwe tayari kufuata kanuni, misingi na vipaumbele vya Jumuia ya Madola vilivyoainishwa katika tamko la Harare la mwaka 1991 na pia nchi iwe tayari kukubaliana na kanuni na mapatano ya Jumuia ya Madola. Hadi sasa Jumuia ina  wanachama wapatao 53 .

Nchi za Jumuia ya Madola ziko Afrika, Amerika, Ulaya na Pacifiki lakini  zinatofautiana kwa maana kwamba zipo zilizo kubwa, ndogo, tajiri na masikini. Nchi 32 ni Jamhuri, 5 ni falme na 16 zinaongozwa na Mawaziri wakuu ambao wanawajibika kwa Malkia wa Uingereza. Jumuia ya Madola haina katiba na hujiendesha kwa kufuata taratibu zinazofahamika, mazoea na matamko mbalimbali au utayari wa kufanya jambo.

Kwa hakika, ““Mtoto acha kupiga mayowe, waache watu waone wenyewe” Ujio wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola Mheshimiwa Patricia Scotland unatosha kumvua chui ngozi ya Kondoo maana sasa watu wanakuja kuona wenyewe na sio porojo.

Ujio wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola unanikumbusha waraka maarufu alioandika gwiji wa fani ya Uhusiano wa Kimataifa Francis Fukuyama mwanzoni mwa miaka ya tisini wenye jina la “ The End of History” akielezea mvutano wa kiitikadi ya Ubepari na Ukomunisti kuwa sasa vita hivyo vimefikia ukingoni kwa Ubepari kushika kasi na Ukomunisti kudhoofika zaidi.

Naam, sasa mwisho wa ‘drip’ tumeuona, hakuna tena ‘kuchomana ndevu’ Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola ameizika ‘drip’ katika kaburi la sahau, kila mmoja kafahamu ukweli wa mambo na kwa msingi huo ndipo pale msemo wa “Kweli ikidhihiri….

Kiongozi makini na mwenye kujali wale anaowaongoza ni lazima awe mfano wa uwajibikaji, uadilifu na uzalendo, katika kipindi cha uongozi wa awamu hii ya saba chini ya Rais Dk. Shein ameonesha uzalendo, upendo na pia kusimamia misingi ya utawala bora.

Kwa mantiki hiyo, Jumuiya ya Madola haikutaka kuwa nyuma katika kumuunga mkono Rais Dk. Shein, kuja kwa Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo kunathibitisha mahaba na ukuruba wa Taasisi hiyo yenye nguvu katika Taasisi za Kimataifa.

MAONI YAKO