Na Mwandishi Wetu

HUWEZI kutaja kuenea kwa umasonia (freemasonry) katika Afrika ya Mashariki bila ya kuitaja Zanzibar, nchi ya kwanza kustaarabika ikitajwa kwamba ustaarabu ndio ulikuwa sababu kubwa ya Zanzibar kuweza kupiga hatua na kutambulika katika sehemu kubwa ya dunia.

Awali ni vyema kutambua historia ya nchi tatu zinazounda chimbuko la Afrika ya Mashariki ambapo kabla ya karne ya 19, eneo la bara (nyika) linalounda Afrika ya Mashariki lilikuwa halijulikani katika sehemu kubwa ya dunia.

Kwa karne kadhaa ilikuwa Zanzibar pekee ndio iliyokuwa ikijulikana pamoja na kuwa na umaarufu mkubwa  kutokana kuwa ni kituo cha biashara  ambacho kikitembelewa na kupokea madau na majahazi kutoka Oman pamoja na meli kubwa kutoka Ulaya, India na sehemu nyengine za dunia.  Umaarufu huo ulitokana pia kuwa ni kitovu cha biashara ya utumwa.

Zanzibar ilimilikiwa na Sultan wa Oman kuanzia karne ya 17, pamoja na maili 10 ndani ya mwambao wa Kenya katika maeneo ya Kipini, katika kianzio cha Mto Tana hadi kusini mwa Mto Umba.  Dunia imekuwa ikiitambua  umuhimu wa Zanzibar kutokana na kuwa kitivo cha biashara kuanzia karne ya 19.  Marekani ikaanzisha ubalozi wake Zanzibar mwaka 1837, ikifuatiwa na Uingereza mwaka 1841 na baadae Ufaransa, Ureno, Italia, Ubelgiji na Ujerumani zikafuatia.

Katika nusu ya pili ya karne ya 19, Uingereza ilizidisha uhusiano wake na Sultani wa Zanzibar, na ilipofika mwaka 1890 uhusiano kati ya Uingereza na Sultani wa Zanzibar uliposhamiri, Zanzibar ikaanza kuwa na watawala wawili kwa wakati mmoja.  Sultani aliyekuwa akiiongoza Zanzibar chini ya uangalizi wa Uingereza.

Sultan Seyyid Hamoud-bin-Mohammed-bin-Said, kati ya karne ya 19, aliwahamasisha wafanyabiashara wa India kuwekeza kwa kiwango kikubwa Zanzibar na kusaidia jitihada za kuinua uchumi wa visiwa vya Zanzibar.  Mbata, vipusa (pembe za ndovu), mazao ya viungo pamoja na watumwa ni miongoni mwa biashara zilizokuwa zikisafirishwa nje ya Zanzibar wakati Zanzibar ikiingiza pamoja na biadhaa nyengine ni pamoja na nguo na nyengine za mapambo (vipuri na shanga).  Inaelezwa kuwa karne ya 19 ndio kipimo cha mafanikio katika biashara ndani ya mwambao wa Afrika ya Mashariki.

Mwishoni mwa karne ya 19, asilimia kuwa ya Waingereza walikuwepo Zanzibar na kwa hatua hii ndio mara ya kwanza umasonia (freemasonry) ulipoibuka kwa mara ya kwanza katika Afrika ya Mashariki, ndani ya Zanzibar mwaka 1904.

Baada ya kinyang’anyiro cha kuigawa Afrika, 1887, Sir William McKinnon kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza alikabidhiwa jukumu la kuiangalia Afrika ya Mashariki na baadae kuanzisha Jumuia ya Uingereza kwa nchi za Afrika ya Mashariki (British East Africa Association) baadae ikaingizwa katika utawala wa Uingereza (Imperial British East Africa – IBEA) iliyopewa jukumu la kuangalia ustawi wa utawala wa  Sultani wa Zanzibar katika maeneo ya bara (nyika) ya ukanda wa Afrika ya Mashariki.  Haikuchukua muda mrefu sana IBEA ikapata ushawishi na ikafanikiwa kuanzisha vituo vya biashara nchini Kenya na katika maeneo yanayozunguka Ziwa Victoria.

Kufuatia Ujerumani kuihodhi Tanganyika, Dr. Karl Peters, aliyekuwa kinara wa Serikali ya Ujerumani kuitwaa Tanganyika, baadae alibadili mwelekeo kwa kuitaka Uganda na kusaini mikataba mbali mbali na viongozi wa makabila ya Uganda kwa lengo la kuitaka Uganda pia iwe sehemu ya Ujerumani.

Hata hivyo, hakuweza kupata ushawishi mkubwa kutoka katika serikali ya Ujerumani, July 1880, Ujerumani na Uingereza walisaini mkataba na kuifanya Uganda nayo pia kuwa chini ya Uingereza.  Hatua hiyo ikaifanya Kenya na Uganda kuwa chini ya himaya ya Uingereza.  Hadi mwaka 1920, Kenya ikawa koloni kamili la Uingereza.

Uganda kwa wakati huo ilikuwa ni miongoni mwa mataifa yenye nguvu sana katika ukanda wa Afrika ya Mashariki na kati kutokana na ustaarabu pamoja na utii wa sheria za Uingereza, lakini zaidi iliheshimika kutokana na kumiliki chanzo cha Mto Nile, mto mrefu kuliko yote barani Afrika.

Kutokana na shinikizo kutoka IBEA, mnamo mwaka 1891, Uingereza ilikubali kufadhili ujenzi wa reli kutoka Mombasa hadi Uganda.  Ujenzi huu ulianza mapema 1890 na kufika Nairobi Mei 30, 1899.  Mervyn Hill katika kitabu chake “Njia ya Kudumu” anaeleza kuwa: “Makao makuu ya reli yakaanzishwa.  Muda mwafaka ukaandaliwa wa kuandaa na ujenzi wa maduka, maeneo ya gereji na ujenzi wa nyumba za makaazi.  Ujenzi wa reli ulitoa mwanya wa kuvunja miamba hadi kufikia Kikuyu.  Mnamo mwezi July 1899, makao makuu ya reli yalihamishwa kutoka Mombasa hadi Nairobi, kipindi hicho ndipo mji wa Nairobi ulipozaliwa.”

Licha ya kufahamika kuwepo kwa hekalu la kwanza la Umasonia katika Afrika Mashariki, Zanzibar.  Historia yaonyesha Umasonia katika Afrika ya Mashariki ulianza kushika kasi baada ya reli kufika Uganda na baadae Nairobi.  Baadhi ya wafanyakazi na viongozi wa kampuni iliyokuwa ikijihusisha na ujenzi wa njia za reli walikuwa ni wakereketwa na waumini wakubwa wa Umasonia, ingawa hakuna kati yao aliyewahikufika katika daraja la juu la uongozi katika Umasonia.

Kumbukizi hizi ndizo zinazotuonyesha jinsi kasi ya ongezekola ushawishi miongoni mwa watu mbali mbali ambao kwa wakati huo walifahamika kuwa ni wasomi na viongozi katika makampuni mbali mbali yaliyokuwepo katika Afrika ya Mashariki jinsi walivyoweza kujihusisha na hamu ya Umasonia, ingawa wengi wakifanya jitihada hizo kwa njia ya siri.

Mnamo mwaka 1900, wakereketwa wa Umasonia walijikusanya pamoja na kujadili uwezekano wa kuwa na hekalu la pamoja la Umasonia, Nairobi.  Wanaumasonia wa Afrika ya Mashariki waliwasiliana na Sir Edward Letchworth, aliyekuwa kiongozi mkuu wa Umasonia.  Akionyesha kusita na hatua ya kuwa na hekalu Nairobi, kutokana na kile kilichoelezwa idadi ndogo ya waumini na wanachama huku ikifafanuliwa zaidi kwamba kati ya wote waliokuwepo Afrika ya Mashariki hakuna kigezo cha kumfanya hata mmoja kuwa kiongozi.

Pia kikwazo kingine kikielezwa kuwa na ugumu wa mawasiliano hasa ya njia ya reli, ambapo ilibainishwa kwamba ni lazima kuwepo na urahisi wa mawasiliano ya usafri wa pamoja na reli kutoka kati mji wa mwambao wa Mombasa hadi Uganda.

Juhudi za kutambulika kwa Umasonia katika Afrika ya Mashariki zilianza kutambulika ingawa katika mazingira magumu, hadi ilipofikia mwaka 1904 baada ya kutumwa waraka wa maombi ya kuanzishwa kwa Hekalu la Amani, kabla ya ombi la Afrika ya Mashariki kukubaliwa Januari 10, 1905.

Hekalu la kwanza Uganda, lililotambulika kama Hekalu la Victoria Nyanza, lilikamilika mwaka 1911.  Miongoni mwa wanachama maarufu walikuwa ni pamoja na Sir Frederick Jackson, aliyeongoza msafara wa IBEA hadi Uganda mwaka 1889; pia aliwahi kuwa Gavana wa Uganda kuanzia 1911-1917.  Alikuwa kiongozi mwanachama wa hekalu kuanzia mwaka 1906 hadi alipohamia Uganda kufanya kazi kikamilifu katika hekalu.

Tanzania, wakati huo ikitambulika kwa jina la Tanganyika, ilikuwa chini ya Ujerumani kuanzia mwaka 1886 hadi 1918; kabla ya kuchukuliwa na Uingereza mara baada ya kumalizika kwa vita vya kwanza vya dunia.  Wakati bado ikitambulika katika himaya ya Ujerumani katika Afrika ya Mashariki, licha ya kuwa chini ya Uingereza, Tanzania ilikabidhiwa kibali cha kuwa na hekalu la Umasonia mwaka 1922.

MAONI YAKO