NA KHAMISUU ABDALLAH

ASKOFU wa kanisa la Tomondo anayedaiwa kufanya shambulio la aibu dhidi ya binti wa mwenye umri wa miaka tisa, amepandishwa katika mahakama ya wilaya Mwanakwerekwe kujibu tuhuma zinazomkabili.

Mshitakiwa huyo Yohana Madai Madai (40) mkaazi wa Tomondo, alifikishwa mahakamani hapo Aprili 6 mwaka huu mbele ya hakimu Mdhamini wa mahakama hiyo Mohammed Amour.

Hati ya mashitaka iliyowasilishwa mahakamani hapo na kusomwa na Mwendesha Mashitaka Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Arafa Zubeir, ilidaiwa kuwa mshitakiwa huyo bila ya halali alimshambulia kiaibu mtoto wa kike mwenye umri wa miaka tisa (jina tunalihifadhi).

Ilidaiwa kuwa Askofu Yohana alimbinya binya  matiti, kumshika kifua na kumvua shungi lake pamoja na kumkamata nywele binti huyo  kitendo ambacho ni kosa kisheria.

Tukio hilo lilidaiwa kutokea Novemba 19 mwaka 2014 majira ya saa 2:00 usiku huko Tomondo wilaya ya Magharibi ‘B’ Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Kosa la shambulio la aibu ni kinyume na kifungu 131 (1) sheria namba 6 ya mwaka 2004 sheria za Zanzibar.

Yohana baada ya kusomewa shitaka hilo alilikataa huku upande wa mashitaka ukidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo tayari umeshakamilika na kuomba kupangiwa tarehe nyengine kwa ajili ya kuwasilisha mashahidi.

Hakimu Mohammed aliiaghairisha kesi hiyo hadi Aprili 19 mwaka huu na kuamuru mshitakiwa huyo kupelekwa rumande hadi tarehe nyengine aliyopangiwa mahakamani hapo.

Pia aliiamuru upande wa mashitaka kuwasilisha mashahidi siku hiyo.

MAONI YAKO